August 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

“See Shared Activity” ya Instagram, Kigezo Cha Kupata Ajira

Mwandishi: Ismail Mayumba

“See Shared Activity” hupatikana kwa urahisi kwa kuingia kwenye wasifu wa mtu, kisha kubonyeza menyu yenye vidoti vitatu. Ukikifungua, kinaonesha muhtasari wa shughuli mlizowahi kushirikiana, ikiwemo ni mara ngapi mmetagiana, maudhui ambayo mmewekeana “likes”, pamoja na maoni (comments) mliyowahi kuandikiana. Hii inatoa picha halisi ya namna mnavyowasiliana na kushirikiana katika mtandao, jambo ambalo linaweza kuwa muhimu sana katika mazingira ya kijamii na kitaaluma.

Katika muktadha wa ajira, waajiri wengi wa sasa hawategemei tu vyeti au uzoefu wa kazi, bali pia huchunguza mwenendo wa mhusika katika mitandao ya kijamii. Hii ni kwa sababu mitandao imekuwa kioo kinachoonesha tabia, mitazamo na maadili ya mtu. Waajiri wanaweza kufuatilia maudhui unayochapisha, aina ya watu unaowafuata, maoni unayotoa, na hata namna unavyoshirikiana na wengine mtandaoni. Kupitia “See Shared Activity”, mwajiri anaweza kuona moja kwa moja aina ya uhusiano uliopo kati yako na taasisi au watu wake, jambo linaloweza kuathiri maamuzi ya kukuajiri.

Kwa mfano, kipengele hiki kinaweza kufichua kama uliwahi kutoa maoni ya heshima au ya kejeli kwa kampuni au viongozi wake. Pia kinaweza kuonesha kama ulikuwa mfuatiliaji wa muda mrefu au umeanza kufuatilia baada ya tangazo la ajira. Taarifa hizi zinaweza kumsaidia mwajiri kutathmini uhalisia wa nia yako na mtazamo wako kuhusu taasisi hiyo. Ikiwa uliwahi kutoa maneno ya dharau au kukosoa kwa njia isiyo ya staha, kuna uwezekano mkubwa wa kuathiri nafasi yako ya kupata ajira.

Vijana ambao tunajua kuwa hatujafikia malengo yetu na tutakutana na watu mbalimbali ili tufike tunapopataka basi tusijimalize mtandaoni kwani inaweza kutukwamisha tunapokutana na hao au taasisi na wakajua kuwa tushawai kuwatukana matusi ya nguoni kwenye mitandao ya kijamii

Kwa hiyo, ni muhimu kutumia mitandao ya kijamii kwa busara, umakini na heshima. “See Shared Activity” ni mfano mmoja tu unaoonesha jinsi teknolojia inavyoweza kufichua tabia ya mtu. Ni jukumu la kila mtumiaji kuhakikisha kuwa anajenga taswira chanya mtandaoni, kwa sababu huenda kile unachokifanya leo kikawa sababu ya kufungua au kufunga mlango wa fursa kesho.