Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Tamasha maarufu la kukuza utamaduni na utalii nchini (Chief Hangaya Utamaduni Festival), linatarajia kufanyika kwa mara ya pili jijini Mwanza Aprili 19,2026.
Akizungumza jana Mkurugenzi wa Cheza Kidansi Entertainment ambao ni waandaaji, Bernard James,alisema,tamasha hilo kwa mara ya kwanza lilifanyika Machi 8,2025 lilifanyika jijini Mwanza katika uwanja wa Furahisha na kuutangaza utamaduni wa makabila mbalimbali nchini, huku likiwavutia zaidi ya watazamaji 5000.
James amesema,tamasha hilo litafanyika kwa siku 2,Aprili 19 na 20,2026 kuanzia sasa 12 asubuhi,katika uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani Mwanza,na kuwapa wadau na wajasiriamali kuuza, kujitangaza na kutengeneza faida kubwa zaidi
Amesema,maandalizi yanaendelea vizuri ili mwaka huu tamasha liweke historia ya kuwavutia watu zaidi ya 10,000 na kuutangaza utamaduni mzuri wa kitanzania, makabila mbalimbali na kuutangaza Mkoa wa Mwanza na vivutio vyake.
Pia amesema kwa mwaka huu wanafanya maboresho kwa kuongeza shughuli zaidi ikiwemo mbio fupi za wakimbiaji zaidi ya 1,000,ngoma za makabila mbalimbali, michezo ya asili zikiwemo sarakasi, bao, mdako, vyakula vya asili vitakavyopikwa na kuliwa uwanjani, maonesho ya mavazi, utani wa makabila, burudani za muziki wa asili na hotuba fupi za wadau.
“Hakuna kiingilio, wananchi wote wanakaribishwa kuja kuburudika, kuelimika, kupata taarifa mpya za utalii, utamaduni, kula vyakula vya asili, kushiriki mbio na kuondoa msongo wa mawazo, kikubwa wavae mavazi ya asili,”amesema James.
Hivyo amewaomba wadau kujitokeza kudhamini tamasha hilo ili wapate nafasi ya kujitangaza, kuuza bidhaa, huduma, kuwafikia wateja wao, kuongea nao na kuwapa elimu ya shughuli zao
Tamasha hilo kwa kiwango kikubwa litautangaza mkoa wa Mwanza pamoja na fursa nyingi zilizopo mkoani humo na Kanda ya ziwa ikiwemo utalii wa utamaduni

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT