May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PM aomboleza kifo cha Lukuvi, Taifa limepata Pigo




Na Joyce Kasiki, Dodoma


WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema tukio la kifo cha Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu William Lukuvi ni gumu kulielewa na kulipokea, akieleza kuwa kifo hubaki kuwa siri ya Mwenyezi Mungu.


Amesema msiba huo umekuja kwa ghafla na kushtua wengi, kwani marehemu alikuwa bado anaendelea na majukumu yake ya kikazi, hata akiwa katika maandalizi ya kikao kabla ya umauti kumfika.


Dkt. Nchemba ameyasema hayo leo 26 Machi 2026 alipofika nyumbani kwa marehemu katika eneo la Area D, jijini Dodoma, ambako alijiunga na familia pamoja na waombolezaji wengine kutoa pole na kuwafariji wafiwa.


Amesisitiza kuwa Taifa limepatwa na pigo kubwa kufuatia kifo cha kiongozi huyo, huku akiwataka Watanzania kuendelea kumuombea marehemu pamoja na kuipa faraja familia, ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu.


Aidha, ameeleza kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mfariji mkuu, na ndiye anayetoa nguvu ya kustahimili majonzi yanayowakabili wafiwa.