April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mawakili kuongoza Kamati mabadiliko ya Katiba Yanga

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SIKU moja baada ya klabu ya Yanga kupokea rasimu ya awali ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, Mwenyekiti wa klabu hiyo Yanga Dkt. Mshindo Msolla kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji wameteua wanachama wake saba kuunda Kamati ndogo ya Mabadiliko Katiba ya Yanga.

Walioteuliwa kuunda Kamati hiyo ni Wakili Sam Mapande, Wakili Raymond Wawa, Wakili Audats Kahendagile na Wakili Mark Anthony pamoja na Mohammed Msumi, Pastory Kiyombia na Debora Mkemwa.

Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kufanya kazi bega kwa bega na Kamati ya Mabadiliko ili kuona vipengele gani vya Katiba vitakavyoathirika na mfumo mpya na kutoa mapendekezo ya Katiba mpya kulingana na mfumo wa mabadiliko tarajiwa.

Jana mara baada ya kukabidhiwa Rasimu ya awali ya mabadiliko ya mfumo wa klabu hiyo, Dkt. Msolla alisema, mara baada ya Kamati hiyo kuteuliowa moja kwa moja itaanza kushughulikia masuala ya Katiba kwani jambo hilo ni lazima lifanyiwe mabadiliko ili kwenda sawa na mapendekezo yaliyopo kwenye rasimu hiyo.