May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makinda Mkuu mpya wa Chuo Kikuu cha Kairuki

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online,Dar

SPIKA mstaafu, Anne Makinda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU) akichukua nafasi ya Dkt. Salim Ahmed Salim.

Hafla ya kumsimika rasmi kwenye nafasi hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki chuoni hapo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chuo hicho Mikocheni jijini Dar es Salam.

Akizungumza mara baada ya kusimikwa kwake, Makinda amesistiza maadili na nidhamu kwenye vyuo vikuu hususana vinavyotoa elimu ya tiba na uuguzi kwa kuwa itasaidia wahitimu wa kada ya afya kutoa huduma zilizo bora na haki.

Pia amesema vyuo hivyo hususani vya binafsi, vibadili changamoto za kiuchumi wazilzonazo na kuwa fursa, ili kuongeza ufanisi na ushindani uliopo kwenye soko.

Amesema mafunzo pamoja na vyeti pekee haitoshi kumtambulisha mhitimu wa chuo kikuu kuwa bora, bila ya kufuatwa kanuni za maadili katika utendaji kazi zao za kuhudumia jamii.

“Nidhamu pekee inaweza kukifanya chuo kuwa chenye ubora, mafanikio pia yanatokana na nidhamu, huwezi kuwatendea visivyo wenzio ukiwa kwenye majukumu yako ukiwa nidhamu. Nidhamu inaogopa,” amesema Makinda.

“Nilikutana na baadhi ya wanafunzi wa chuo hiki, nikaona kabisa kna nidhamu, hiyo ni muhimu sana, nidhamu maadili kwa wanafunzi ni kitu cha kwanza. Nilipokuwa India siku za nyuma, baadhi ya wadau waliniambia watafungua chuo cha wauguzi, kwa sababu wnasikia baadhi yao hawana nidhamu.”

“Pamoja na wahitimu wa sekta ya afya baadhi yao kutokuwa na ajira, bado watoa huduma hawa wanahitajika kwenye jamii na taifa kwa ujumla.”

Anne Makinda

Kadhalika, Makinda alitoa wito kwa chuo hicho kubuni vyanzo vya mapato, badala ya kutegemea chanzo pekee cha ada kutoka kwa wanafunzi, huku akishukuru chuo hicho kwa kumchagua kuwa mkuu wa chuo, akichukua nafasi ya Balozi Salim Ahmed Salim.

“Ni Mungu amenichagua kuwa katika nafasi hii, ingawa ukistaafu unahitaji kutulia na majukumu, nikakubali sababu najua Mungu kupitia chuo hiki ndio amenichagua. Lakini mimi nakawambia nawaangalia ninyi sababu historia ya hospitali hii naijua, mna ushirikiano, upendo na nia, licha ya kuondoka mwanzilishi, marehemu Kairuki.

“Mfumo aliouacha umefanya chuo hiki kiendelee kuwepo. Nidhamu maadili naiona kwa wanafunzi wenu mnaowafundisha, hata ukiwa nje huko, kwa sababu masomo ni yale yale katika vyuo vingine ila ninyi mnanidhamu.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa chuo hicho, Kokushubila Kairuki, amesemakuwa anaiomba serikali iangalie naman ya kuvisaidia vyuo binafsi kwa kuwapatia fedha ili kuinua ufanisi wa vyuo nchini.

“Nina imani wahitimu wa vyuo binafsi, ikiwamo Kairuki wakitoka hapa wanakwnda kuhudumia jamii hivyo tunaiomba Serikali isaidie kutoa fedha kwa vyuo binafsi. Pendekezo hili linaanzia kwa mkuu wetu mpya, Makinda, tunafahamu uzoefu ulionao katika uongozi na una ushawishi,” amesema Kairuki.