April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli

Magufuli atema cheche mapambano ya CORONA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhusu hali ya ugonjwa wa Corona nchini, ambapo kabla ya kikao hicho Mhe. Rais  amemuapisha  Prof. Mabula Daudi Mchembe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto .Hafla iliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita , Aprili 22, 2020.

Na Mwandishi Wetu

RAIS John Magufuli, ameelekeza hatua za kuchukua katika kupambana na Corona, huku akisisitiza kwamba hatafunga jiji la Dar es Salaam kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakishauri.

Rais Magufuli alitoa maelekezo hayo jana wakati wa kikao chake  na viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kilichofanyika Chato, mkoani Geita jana.

Rais Magufuli alisema kumekuwepo na papara ya watu wetu wakipita kwenye mabasi na kufanya fumigation (upuliziaji dawa), akisema hakuna furmigation yoyote inayoweza kuua corona.

“Kama kungekuwa kunafanyika furmigation na corona wanakufa, basi nchi za wenzetu wasingekuwa wanaendelea kufa,” alisema Rais Magufuli na kusisitiza; “Furmigation iliyokuwa inafanyika Dar es salaam ni upuuzi mtupu. Fumigation inaua mende, viroboto vya mbu, niliwaona viongozi wanafanya furmigation kuua corona.”

Rais Magufuli alisema ni lazima tujiulize, je hizo fumigation zinazofanyika zikiwa na corona? “Dar es Salaam walipofanya fumigation wagonjwa wa corona ndipo wameongezeka, ndiyo maana nimewaita nyie viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama ili mkawaulize hao nani aliwaagiza wafanye hizo fumigation?” Alisema Rais Magufuli akiwaelekeza viongozi wa Ulinzi na Usalama.

Kufunga Dar

Rais Magufuli, alisema wapo wanaotoa mawazo ya kuifunga Dar es Salaam, mawazo ambayo ameyakataa akisema  Dar es Salaam ndiyo centre (Kituo) cha mapato.

Alisema  zaidi ya asilimia 80 ya mapato yanapatikana, Dar es Salaam “Sasa unapoifunga Dar es Salaam watu wasifanye biashara? Watu wasilete mazao yao Dar es Salaam?  Tuendelee kufanya biashara, lakini sio kuwafunguia Dar es Salaam,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Dar ina watu milioni sita wote ukiwafungia, na ikitokea Mwanza na Mbeya nako unawafungia? “Dar kama watu ni milioni sita uwezekano wa kuwa na wagonjwa wengi ni kubwa,” alisema Rais Magufuli.

Alionya kuhusiana na kasumba iliyoanza kwa Watanzania ya kuwaogopa watu wa Dar es Salaam akisema hiyo ni kasumba mfu. “Corona tutaishinda kwa ushirikiano, kwa kumaliza hofu, kwa kumtanguliza Mungu kama tulivyoshinda vita nyingine,” alisema Rais Magufuli.

Alisema jana alimsikiliza Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) akisema kuna wagonjwa 284. Rais Magufuli alionesha wasiwasi wa kuchanganya takwimu za wagonjwa wanaopona, hivyo ameagiza takwimu hizo nazo zitangazwe ili wananchi waondolewe hofu.

Alifafanua kwamba taarifa alizonazo yeye watu waliokufa corona ni 10, hivyo watu wasijengewe hofu kwa kila anayekufa amekufa na Corona.

“Ina maana kila anayekufa ni Corona? Je malaria imeacha kuua?”Alihoji Rais Magufuli na kuwataka Watanzania wasiwe na hofu ya namna hiyo.

Amemuagiza Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Mabula Mchembe, akahakikishe  taarifa za watu wanaopona ziwe zinatolewa na watu sio kujengewa hofu.

Wanaowekwa Karantini

Akizungumzia watu wanaowekwa karantini kwenye Hosteli za Magufuli Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Magufuli, aliagiza suala hilo liangaliwe upya, kwani hakuna sababu ya watu kuwakalisha kwenye hosteli hizo siku 20 wakati hawana ugonjwa.

“Tushughulike zaidi na wagonjwa badala ya kuhangaika na watu ambao hawana ulazima,” alisema.

Taasisi za fedha

Kupitia mazungumzo yake na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Rais Magufuli aliziomba taasisi za fedha za kimataifa ziangalie uwezo wa nchi za Afrika Kiuchumi kwani ni mdogo.

Alishauri taasisi hizo ikiwemo Benki ya Dunia (WB) kuomba kuzisamehe madeni nchi za Afrika ili fedha hizo zitumike kwenye mapambano dhidi ya Corona.

Alisema anajua WB wametoa ofa kwa nchi zinazosumbuliwa na corona kukopa fedha, lakini ameshauri nchi hizo zisamehe madeni walizokopeshwa ili yatumike kupambana na corona badala ya nchi hizo kuongezewa mzigo wa madeni.

Alitoa mfano kwamba kila mwezi Tanzania inatumia sh. bilioni 700 kulipa madeni kwa taasisi mbalimbali na kwamba imekuwa ikitumia kati ya sh. bilioni 200- 300 kulipa deni la Benki ya Dunia kwa mwezi.

“Kama wana nia ya kutusaidia watusamehe madeni hata kwa asilimia ili fedha hizo zisaidie katika mapambano ya Corona badala ya kuziongezea mzigo mwingine wa kukopa,”alisema Rais Magufuli. Alitoa wito kwa nchi nyingi za Afrika zishirikiane kuziomba taasisi za fedha kusamehe nchi za Afrika madeni hayo.

Upotoshaji mitandaoni

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amekemea vikali taarifa za upotoshaji kuhusu ugonjwa wa corona. “Watu wa mitandao wajizuie kuandika habari za uongo na wananchi wapuuze,” alisema na kusisitiza kwamba mitandao mingine haipo hapa nchini.

Alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kushughulika na watu wanaotoa taarifa za uongo kuhusu corona.

Tiba asili

Wakati huo huo, Rais Magufuli aliwaomba Watanzania kutumia njia nyingine za asili kama kujifukizia kwa ajili ya kukabiliana na Corona. Ametoa wito kwa Wizara ya Afya kufafanua ni kwa namna gani kujifukizia kunaweza kusaidia katika mapambano ya Corona.

“Tuendelee kutumia njia za asili kama kujifukizia ili kupunguza corona,” alisema. Mbali na kushauri njia za asili kutumika, alihimiza Watanzania waendelee kuchukua hatua za tahadhari za ugonjwa huo.

Wanasiasa

Kuhusu wanasiasa Rais Magufuli alisema ugonjwa wa Corona umekumba mataifa yote, hivyo wakati huu ni wakati wa kushikamana amepongeza wale wote walioonesha kushikamana kupambana na ugonjwa huo.

Rais Magufuli alivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuilinda nchi yetu hasa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya COVID-19.

“Nimekubaliana na hatua mnazoendelea kuzichukua katika kipindi hiki. Nawapongeza viongozi wa Dini na Watanzania kwa ujumla kwa kuitikia wito wa kuliombea taifa kwa siku tatu dhidi ya ugonjwa wa COVID-19, nina amini Mungu wetu ni wahuruma atatusikiliza na siku moja tutalishinda hili gonjwa,”alisema.

Pia aliwashukuru kwa kwenda Chato kumpa ‘briefing’ za jinsi tunavyoendelea kupambana na Corona. “Nimekubaliana na hatua mnazoendelea kuzichukua katika kipindi hiki, Napenda kushukuru Watanzania ambao kwa nyakati za maombi tulizotangaza kwa siku 3, wote walishiriki

Nawapongeza madaktari, manesi na wahudumu wote wa sekta ya afya nchini ambao kila mmoja katika maeneo yao ya kazi wameendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa mbalimbali na wagonjwa wa COVID-19.

Endeleani na moyo huo wa uzalendo, mnafanya kazi ya Mungu ya kuwahudumia Watanzania, msivunjike moyo, Serikali ninayoiongoza ipo pamoja nanyi, ninatambua kazi kubwa mnayoifanya,”alisema