July 3, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu wa Baraza la Ulamaa, Shekhe Hassan Chizenga

Baraza la Ulamaa BAKWATA laagiza Maimamu kupunguza urefu wa swala

Na Irene Clemence

BARAZA la Ulamaa BAKWATA Taifa limewataka Maimamu wote nchini kupunguza urefu wa swala zote za Faradhi na badala yake zisaliwe kwa ufupi katika kipindi hiki cha kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Pia Baraza hilo limeagiza swala ya Tarawehe ipunguzwe iwe rakaa 10 badala ya 20 kama ilivyokuwa awali ikiwa ni hatua za kukabiliana na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19).

Hayo yamesemwa Jijiji Dar es Salaam jana Shekhe Hassan Chizenga, wakati akizungumza waandishi wa habari kuhusiana na tamko la Baraza la Ulamaa BAKWATA kuhusiana na namna ya kukabiliana na Corona sambamba na utekelezaji wa ibada hususani katika kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Amesema hatua hiyo imekuja baada ya Baraza hilo kufanya kikao chini ya uenyekiti Mufti wa Tanzania Shekhe Abubakari Zuberi kwa lengo la kutafakari hatua za kuzingatia kukabiliana na Virusi vya COVID-19 nchini.

Pia amesema Baraza hilo limesitisha utaratibu wa kufuturisha kwa pamoja na badala yake wale wenye nia ya kufutilisha watu wasio kuwa na uwezo, waandae futari za kubeba mikononi (take away) au kuwapa watu chakula wapike wenyewe ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.