April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini waomba Mungu atuepusha na Corona

Na WAMJW Dar Es Salaam

VIONGOZI wa madhehebu mbalimbali ya dini wameendesha maombi maalum ya kuiombea nchi dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona. Maombi hayo yamefanyika katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam jana ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wakiongoza maombi hayo ya kitaifa baadhi ya viongozi wa dini wamemshukuru Rais John Magufuli kwa kuruhusu kuabudu na kuliombea taifa dhidi ya janga la Corona nchini.

Kwa upande wake Mufti wa Tanzania Shekhe Abubakari Zubeir alimwomba Mungu  kuondosha mtihani huo wa Corona amabao umeitikisa dunia kwasasa na kuomba waumini kuendelea kuomba kwa ajili ya kuondokana na janga hilo.

Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Jude Thadeus Rwaichi alisema kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi wa maisha ya mwandamu hivyo ni budi kumuomba yeye ili atupitishe salama na kuondokana na janga hili la Corona.

Pia iongozi wengine waliongoza maombi walitoka katika  Jumuiya ya Kikristo Tanzania, Jumuiya ya Mabohora, Kanisa la Pentekoste, Kanisa la Wasabato, Mwakilishi wa Mufti wa Zanzibar na wafuasi wa madhebu ya Budha Tanzania.

Maombi haya dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayoambukizwa na virusi vya Corona ni mwendelezo wa maombi ya kitaifa yaliyoitishwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili, 2020 kote nchini.

Mapema tarehe 9 Aprili, 2020 Viongozi wa Dini na baadhi ya Viongozi wa Serikali walikutana jijini na Dar es Salaam na kuazimia kufanyika kwa maombi maalum ya kitaifa yanayoshirikisha waumini wa madhebu yoye nchini ili kuiombea nchi dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.