June 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kwagila apongeza TPDC Kuendeleza Matumizi Gesi Asilia


Ja Joyce Kasiki,Dodoma

AFISA kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Eugine Isaya, amesema shirika hilo linaendelea kutekeleza jukumu lake la kutafuta, kuendeleza na kuzalisha mafuta na gesi nchini, sambamba na kusambaza gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ya wananchi na sekta za uzalishaji.


Isaya ametoa maelezo hayo Juni Mosi mwaka hui mbele ya Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagila, alipotembelea banda la TPDC wakati wa ufunguzi maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani.


Alisema TPDC, ambalo ni shirika la serikali lililo chini ya Wizara ya Nishati, linashiriki maadhimisho hayo kutokana na mchango wake katika uzalishaji na usambazaji wa gesi asilia, ambayo ni moja ya nishati safi inayosaidia kuhifadhi mazingira.


“Moja ya bidhaa tunazozalisha na kuzisambaza kwa sasa ni gesi asilia inayotumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani, viwandani, kwenye magari na matumizi mengine ya kiuchumi.

Katika maonesho haya tumekuja na gari la mfano linalotumia nishati ya gesi asilia ili wananchi waweze kuona faida na matumizi ya teknolojia hii,” alisema Isaya.


Aliongeza kuwa hadi sasa Tanzania ina magari takribani 15,500 yaliyounganishwa na kutumia nishati ya gesi asilia, huku vituo 17 vya kujaza gesi hiyo kwenye magari vikiwa vinaendelea kutoa huduma katika maeneo mbalimbali.


Aidha, alisema Serikali kupitia TPDC ipo katika mkakati wa kupanua huduma ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro na Arusha ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hiyo.


“Kwa sasa huduma ya gesi asilia inapatikana katika mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Dar es Salaam. Lengo la upanuzi huu ni kuongeza upatikanaji wa nishati safi na rafiki kwa mazingira kwa watumiaji wengi zaidi nchini,” alieleza.


Kwa upande wake, Naibu Waziri Reuben Kwagila amelipongeza TPDC kwa jitihada zake za kuhamasisha matumizi ya gesi asilia na kuendeleza nishati safi nchini.


Alisema kazi inayofanywa na shirika hilo ina mchango mkubwa katika kulinda mazingira, kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira na kusaidia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia matumizi ya nishati mbadala na endelevu.

Kwagila alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za matumizi ya gesi asilia ili kuongeza matumizi yake katika sekta mbalimbali na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira.