
Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Kilimanjaro
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza Serikali kwa kumaliza changamoto ya wanafunzi waliokuwa wanasoma katika Shule ya Msingi Msamadi, iliyokuwa umbali wa takribani kilometa 12 kutoka kijijini kwao.
Imeelezwa kuwa, kutokana na umbali mrefu, wanafunzi walilazimika kuvuka barabara kuu kila siku, jambo liliosababisha ajali za mara kwa mara na kuhatatarisha usalama wao, huku ikitolewa takwimu ya takribani wanafunzi 10 wamefariki wakati wakivuka barabara hiyo, hivyo Serikali iliona umuhimu wa kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi ili kuwaondolea adha hiyo.

Akizungumza na wananchi wa Kwasadala, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, leo Mei 31, 2026 alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa shule hiyo, aliwataka wananchi hao kulinda miundombinu ya shule hiyo iliyojengwa kwa thamani zaidi ya Sh. Mil 300 kwa ajili ya manufaa yao.
Pia aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia anazoendelea kufanya katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu ya barabara nk, huku akimtaraja Rais huyo kuwa ndiye aliyevunja rekodi kwa kufanya mambo makubwa nchini katika kipindi cha mida mfupi.
“Tumeelezwa kuwa hapo awali wanafunzi walikuwa wakitembea kwa umbali mrefu kwenda shule na wanafunzi 10 tumeambiwa walifariki kwa kugongwa na magari wakati walipokuwa wakienda shule.

Hivyo, niwaombe ndugu zangu tuilinde miundombinu hii kwa manufaa ya watoto wenu, lakini pia niwaombe muendelee kuunga mkono juhudi za Rais wetu kwani ndiye Rais aliyevunja rekodi ya kufanya mambo makubwa nchini ndani ya muda mfupi”, amesema kihongosi.
Shule ya Kwasadala ina madarasa saba ya shule ya msingi, madarasa mawili ya elimu ya awali, matundu ya vyoo 19, jengo la utawala na uwanja wa michezo, huku fedha za ujenzi wa shule hiyo ikiwa imetoka Serikali kuu na wanakijiji kuchangia nguvu kazi kwa kuchimba misingi ya majengo pamoja na kujitolea eneo la ujenzi.



More Stories
DC,Chirukile ziarani Kongo kujenga mahusiano ya Kidiplomasia,uchumi
NMB yaiweka Tanzania kwenye ramani ya Mitaji Cambridge
SKA yahamasisha waandishi wa habari kuwania Tuzo