Na Mwandishi wetu,Timesmajira
WAANDISHI wa habari nchini wamehamasishwa kujitokeza na kushiriki katika kuwania Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo za Samia Kalamu Awards (SKA) 2026, msimu wa pili, zinazolenga kutambua na kuthamini mchango wao katika kuhabarisha umma kuhusu maendeleo ya taifa.
Tuzo hizo zimeandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) pamoja na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari(JAB)
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema Mchakato wa kuwasilisha kazi hizo umeziduliwa rasmi Mei 31, 2026 na unatarajia kuhitimishwa Juni 30, 2026 katika tovuti ya Samia Kalamu Awards.
Amesema maandalizi ya utoaji wa tuzo hizo yameanza rasmi ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Samia Suluhu Hassan kwa lengo kutambua, kuthamini na kuhamasisha uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora yanayochangia kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha jamii huku yakikuza taswira chanya ya taifa kupitia habari za maendeleo.
“Mwaka huu Samia Kalamu Awards 2026 zitahusisha makundi matatu ambayo ni Tuzo Maalumu za Kitaifa, Tuzo za Vyombo vya Habari pamoja na Tuzo za Kisekta,” amesema.

Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa tuzo hizo mwaka 2025, zimekuwa kichocheo muhimu cha kuhamasisha uandishi na uandaaji wa habari na makala zinazozingatia utafiti na uchambuzi wa kina wa masuala ya maendeleo, uwajibikaji, uzalendo na ujenzi wa taswira chanya ya taifa.
Amesema, mwandishi anayetarajia kushiriki anatakiwa kuwa raia wa Tanzania, kuthibitishwa na JAB kwa Tanzania Bara au kuwa na kitambulisho cha mwandishi wa habari kwa upande wa Zanzibar, pamoja na kutokuwa na rekodi ya kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai.
Aidha, kazi zitakazoshindanishwa zinapaswa kuwa zimechapishwa, kutangazwa au kurushwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza kati ya Julai 1, 2025 na Juni 30, 2026.
Pia zinapaswa kuwa zimefanyiwa utafiti wa kina, kutumia angalau vyanzo vinne vya habari na kutokuwa zimeshawahi kushindanishwa katika tuzo nyingine.
Amesema kazi hizo zinapaswa kuibua simulizi za wananchi kuhusu namna miradi ya maendeleo ilivyofungua fursa na kubadili maisha yao huku zikizingatia ulinzi wa haki-miliki na haki shiriki.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TAMWA Dkt Kaanaeli Kaale amesema Waandishi wa habari nchini wana nafasi kubwa katika kuharakisha maendeleo ya taifa kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu miradi na huduma mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali.
Amesema maendeleo ya taifa huanzia katika ngazi ya familia na kaya, hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi, hususani wanawake wa vijijini, wananufaika na maendeleo yanayotekelezwa.
“Habari za maendeleo ni chachu ya maendeleo ya taifa. Tunapozungumzia maendeleo ya taifa, ni lazima tuangalie namna yanavyogusa maisha ya wananchi mmoja mmoja, hasa wanawake ambao mara nyingi hubeba jukumu kubwa la familia,” amesema.
Naye Mkurungezi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula amesema washiriki wa tuzo hizi, wanapaswa kuwa wanatambuliwa na kuthibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.
“Hili ni jambo muhimu sana kwa sababu ni takwa la kisheria na hatuwezi kulipuuzia. Kwa hiyo, ni muhimu washiriki wote wawe wameidhinishwa na kutambuliwa rasmi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa”amesema

More Stories
DC,Chirukile ziarani Kongo kujenga mahusiano ya Kidiplomasia,uchumi
NMB yaiweka Tanzania kwenye ramani ya Mitaji Cambridge
Zaidi ya Mil.300 yaondoa adha Km,12 Hai