April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kilo 1,983 dawa za kulevya zakamatwa nchini

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema kipindi cha mwezi Machi 2026, imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika nchini kote.

Haya yamesemwa Aprili 13, 2026, jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Amesema, mafanikio hayo yanatokana na mkakati wa Mamlaka kujikita zaidi katika operesheni za mashambani na kwenye njia kuu za usafirishaji baada ya kuimarisha udhibiti bandarini na mipakani.

“Katika kipindi cha mwezi Machi 2026, tumekamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa za kulevya aina mbalimbali, pamoja na kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu ambazo zingetumika kuzalisha dawa hizo,” amesema Lyimo.

Amesema, ongezeko kubwa limeonekana katika ukamataji wa mirungi, ambapo pekee yake ilifikia kilogramu 1,267.12 sawa na asilimia 64 ya dawa zote zilizokamatwa katika kipindi hicho.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, operesheni hizo pia zimefanikiwa kukamata vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, zikiwemo aina za benzodiazepine na opioid kama vile tramadol na codeine, ambazo hutumika vibaya na kusababisha uraibu.

“Tumebaini kuwepo kwa mbinu mpya za usafirishaji wa dawa za kulevya, ikiwemo kuficha kwenye mizigo ya nguo za mitumba, matunda kama maembe, pamoja na ndani ya vyombo vya usafiri ikiwemo mifumo ya hewa (AC) kwenye mabasi,” ameongeza.

Katika operesheni hizo, Kamishna Lyimo amesema Jijini Dar es Salaam, katika eneo la Tegeta Kibo, walikamata kilogramu 101.2 za mirungi zilizokuwa zimefichwa katika basi la abiria aina ya Yutong la kampuni ya Abood lenye namba ya usajili T 181 EMJ.

Basi hilo lililokuwa likifanya safari zake kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania.

Amesema, Dawa hizo zilifichwa katika maeneo mbalimbali ya basi hilo ikiwemo ndani ya mfumo wa hewa (AC) kwa lengo la kukwepa kugundulika.

Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni dereva wa basi hilo Ramadhan Mohamed (52), Salma Sanga (26) kondakta,
Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39)

Aidha, amesema ekari 55.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa na watuhumiwa 77 kukamatwa kuhusiana na makosa hayo.

Kamishna Lyimo amesema Mamlaka inaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi nyingine za udhibiti ili kuvunja mitandao hiyo mipya.

“Tutahakikisha tunachukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya bila kujali hadhi yake katika jamii,” amesisitiza.

Mbali na hivyo, Kamishna Lyimo ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za wahalifu na kuendelea kulinda jamii dhidi ya athari za dawa za kulevya, hususan katika maeneo ya taasisi za elimu.