Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPPUNI. ya Mawasiliano Yas kwa kushirikiana na Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania, imefanya kambi maalum ya huduma za matibabu ya macho.
Kambi hiyo iliwahudumia zaidi ya wakazi 4,000 katika Wilaya ya Iramba, mkoani Singida.
Ushirikiano huo unaakisi dhamira ya Yas katika kuwekeza kwenye ustawi wa jamii, sambamba na jitihada za kuboresha afya ya macho.
Lakini pia, kupunguza matatizo ya uoni yanayowakabili wakazi wa maeneo ya vijijini wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Akifungua kambi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ameipongeza Yas na Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania katika kufanikisha zoezi hilo, akibainisha kuwa matatizo ya macho bado ni changamoto kubwa katika jamii.
Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kunufaika na huduma hizo za bure, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za kijamii una mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya nchini.
Mratibu wa kambi hiyo, Ain Sharif, amesema huduma hizo za bure zinajumuisha uchunguzi wa macho, utoaji wa dawa na miwani kwa waliokutwa na tatizo, ushauri wa kitaalamu pamoja na upasuaji mdogo wa mtoto wa jicho kwa wagonjwa watakaobainika kuwa na tatizo hilo.
Ameongeza kuwa, wagonjwa watakaohitaji matibabu ya juu zaidi watapewa rufaa ili waweze kuendelea kupatiwa huduma katika vituo vya afya vyenye uwezo mkubwa, huku kipaumbele kikitolewa kwa watoto ili kuwawezesha kurejea masomoni bila changamoto za uoni.
“Lengo la kambi hii ni kuwafikia wananchi wengi ambao hawana uwezo wa kupata matibabu ya macho.
“Tunatarajia kuhudumia zaidi ya watu 4,000 ndani ya siku hizi tatu, na tayari timu ya madaktari bingwa na wauguzi imewasili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi,” amesema Sharif.
Kwa upande wake, Meneja Mauzo wa Yas Mkoa wa Singida, Emmanuel Kaminyonge, amesema ushiriki wa Yas katika zoezi hilo, ni sehemu ya dhamira yake ya kuendelea kuwa karibu na jamii na kuchangia maendeleo ya kijamii nje ya huduma za mawasiliano.
“Yas tunaamini afya bora ni msingi wa maendeleo ya jamii. Kupitia ushirikiano huu, tunalenga kusaidia kuboresha maisha ya wananchi wa Iramba na maeneo jirani kwa kuwapatia huduma muhimu za afya ya macho bila gharama,” amesema Kaminyonge.

More Stories
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni