August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UDOM yabuni kifaa cha Utrasound bila kutumia mtandao

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma


CHUO Kikuu   cha Dodoma (UDOM) kimebuni kifaa cha ultrasound kupitia mradi wa safiri,kinachofanya kazi bila kutumia mtandao, hatua inayotarajiwa kurahisisha huduma za uchunguzi wa wajawazito katika maeneo ya vijijini na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Hayo yalisemwa na mtafiti wa mradi huo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Rajab Simba, alipotambulisha teknolojia hiyo katika maonyesho ya wakulima na wafugaji Nanenane Nzuguni jijini Dodoma

Aliaema kuwa kifaa hicho kimetengenezwa ili kumwezesha mhudumu yeyote wa afya, ikiwemo nesi au clinical officer, kufanya uchunguzi wa awali wa mimba hata katika vituo visivyo na mtaalamu wa ultrasound.

Alisema kifaa hicho hufanya kazi bila kutumia bando au huduma ya intaneti na hutoa majibu ya haraka yanayomsaidia mhudumu wa afya kubaini umri wa mimba na hali ya mama mjamzito ili kuchukua hatua stahiki kwa wakati.

“Kifaa hiki kinaweza kutumika na mhudumu yeyote wa afya,hufanya kazi bila intaneti na hutoa majibu yanayosaidia kubaini hali ya ujauzito mapema ili kupunguza hatari ya kupoteza maisha ya mama na mtoto,” alisema Simba.

Alieleza kuwa teknolojia hiyo itapunguza rufaa zisizo za lazima ambazo huwawalazimu wajawazito kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali zenye huduma za ultrasound.

Kwa mujibu wa Simba, badala ya mama kupewa rufaa kutoka kituo kimoja kwenda kingine kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida, huduma hiyo itapatikana katika zahanati au kituo cha afya husika, hivyo kupunguza muda, gharama za usafiri na usumbufu kwa wagonjwa.

Alisema rufaa zitatolewa pale tu uchunguzi wa awali utakapobaini dalili za hatari zinazohitaji uchunguzi wa kina kwa kutumia vifaa vya ngazi ya juu.

Simba alisema mradi wa huo umeanzishwa kwa lengo la kuwafikishia wajawazito huduma za uchunguzi karibu na maeneo wanayoishi, hususan vijijini ambako kuna upungufu wa wataalamu wa ultrasound na changamoto ya upatikanaji wa huduma hizo.

Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yanatarajiwa kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa kuwezesha uchunguzi wa mapema na kuongeza fursa ya kuokoa maisha ya mama na mtoto.