Na Joyce Kasiki, Dodoma
MENEJA Masoko na Uhamasishaji wa Mfuko wa SELF Microfinance Fund, Linda Mshana, amewataka vijana, wajasiriamali, wakulima, wafugaji na wafanyakazi wa taasisi mbalimbali kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na mfuko huo ili kujiajiri, kuanzisha viwanda vidogo, kuongeza thamani ya mazao na kuwekeza katika biashara zinazochochea matumizi ya nishati safi.
Mshana alitoa wito huo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma, ambapo alisema SELF Microfinance Fund imejikita katika kutoa elimu ya fedha na mikopo yenye masharti nafuu kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi kupitia shughuli za uzalishaji.
Alisema mfuko huo unatoa fursa kwa vijana wanaotaka kuanzisha biashara mpya, zikiwemo biashara za kahawa, usindikaji wa mazao na shughuli zinazohusiana na nishati safi, ikiwemo uzalishaji na uuzaji wa majiko banifu.
“Tunawahamasisha vijana kutumia fursa zilizopo,unaweza kujifunza kutengeneza kahawa au bidhaa nyingine, kupata mkopo na kuanzisha biashara yako. Hii inachangia kuongeza ajira, kukuza kilimo cha kahawa na kuongeza thamani ya mazao ya ndani,” alisema Mshana.
Alieleza kuwa SELF Microfinance Fund inaendelea kuunga mkono matumizi ya nishati safi kwa kufadhili biashara zinazochangia utunzaji wa mazingira, huku ikiwasaidia wananchi kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo kuanzia uzalishaji, uchakataji, usafirishaji hadi masoko.
Mshana alisema mfuko huo tayari umetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 400 kwa wanufaika mbalimbali nchini, huku zaidi ya wananchi 600,000 wakinufaika na huduma hizo, na kwamba lengo ni kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Alifafanua kuwa masharti ya kupata mkopo ni rafiki, ambapo mwombaji anatakiwa kuwa na shughuli ya uzalishaji au biashara iliyodumu kwa angalau mwaka mmoja ili kustahili kupata huduma hiyo.
Mbali na mikopo, alisema SELF Microfinance Fund hutoa elimu ya fedha inayowawezesha wananchi kupanga uwekezaji, kukuza mitaji, kutumia mikopo kwa ufanisi na kuepuka madeni yasiyo ya lazima.
Aidha, alisema mfuko huo unatoa huduma za bima, ikiwemo bima ya usafirishaji wa mazao na bidhaa, inayolinda mali za wafanyabiashara dhidi ya hasara zinazoweza kujitokeza wakati wa usafirishaji.
Mshana aliwataka wananchi kutembelea banda la SELF Microfinance Fund katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu, ushauri na kufahamu fursa mbalimbali za mikopo pamoja na huduma nyingine zinazotolewa kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo yao.

More Stories
Mbolea ya fomi yaleta neema kwa wakulima
Msichana Initiative yawajengea uwezo Waandishi wa habari kupinga ndoa za Utotoni
Takwimu sahihi zatajwa nguzo muhimu maendeleo ya Taifa