April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Matumizi ya Stendi kuu ya mabasi Katumba kuanza rasmi Julai Mosi mwaka huu

Na Israel Mwaisaka, Rukwa

‎Serikali imeahidi kuboresha sekta ya usafiri na usafirishaji katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa kuanza rasmi matumizi ya Stendi Kuu ya Mabasi Katumba kuanzia Julai 1, 2026.

‎Hatua hiyo itaenda sambamba na kufungwa kwa stendi ya Sokomatola ili kupisha utekelezaji wa mipango mingine ya maendeleo iliyokusudiwa na Serikali.



‎Mpango huo unakuja kufuatia maombi ya Wananchi yaliyotolewa Machi 8, 2026 wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ambapo walisisitiza matumizi kamili ya stendi ya Katumba iliyogharimu Shilingi Bilioni 8.993.

‎Akizungumza katika kikao na wadau wa usafirishaji Aprili10, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Nassir Kirusha, amewapongeza wadau hao kwa juhudi zao za kujiletea maendeleo na kusisitiza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu na fursa za maendeleo kwa lengo la kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.



‎Amesema matumizi ya stendi ya Katumba yataongeza ajira kwa vijana kupitia shughuli za bodaboda, bajaji na usafiri wa ndani (haisi), pamoja na kukuza mzunguko wa fedha kupitia biashara za wajasiriamali.

‎Kwa upande wao wadau wa usafirishaji wameipongeza Serikali kwa mipango hiyo, wakieleza kuwa matumizi kamili ya stendi ya Katumba ni hatua muhimu itakayochochea maendeleo endelevu ya wananchi.



‎Kikao hicho kimehusisha wadau mbalimbali wa usafirishaji, wajasiriamali pamoja na wawakilishi wa wafanyabiashara (machinga).

‎Aidha, Serikali inaendelea na mipango ya kujenga stendi ndogo katika maeneo ya Isofu na Kanondo ili kurahisisha huduma za usafiri katika maeneo ya pembezoni.