March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga (kushoto) akizungumza katika uzinduzi wa programu.

Kilimo cha kidigitali kuinua maisha ya wana Iringa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga amesema, uzinduzi wa programu ya yaraConnect utasaidia Serikali na wadau wa kilimo katika kufikia malengo waliyojiwekea katika kuhakikisha wakulima wanafanya kilimo chenye tija.

Ameyasema hayo katika uzinduzi wa programu ya yaraConnect kwa mkoa huo mjini humo ambapo alisisitiza kuwa,wakulima wengi mkoani humo na kwa Tanzania kwa ujumla wanafanya kilimo cha mazoea, hivyo si rahisi kuweza kuleta matokeo yenye tija.

“Ili kufanya kilimo chenye tija tunahitaji elimu na taarifa sahihi kuhusu hali ya hewa, misimu mbalimbali ya mwaka na matumizi bora ya pembejeo za kilimo, uzinduzi huu wa programu ya yaraConnect utamkomboa mkulima na pia kurahisisha utendaji kazi wa maofisa ugani wetu ambao bado walipo hawatoshelezi.

“Dunia ya sasa hivi ni dunia ya kidigitali, hivyo hatuna budi kwenda sambamba na mabadiliko ya kidigitali yanayotokea, ni matumaini yetu kama serikali ya Mkoa wa Iringa na wadau wote wanaohusika tutaitumia App hii vizuri kwa malengo ya kupata ufanisi ili kuleta maendeleo.

“Natoa wito kwa makampuni mengine ya pembejeo za kilimo kuiga mfano wa Yara kwani wamekuwa mstari wa mbele katika ubunifu ndio maana bidhaa zao zinapendwa sana na wakulima sio kwa Iringa tu bali nchi nzima.

“Mkoa wa Iringa tunakuja na mapinduzi mazito sana ya kuhakikisha kuwa tunaboresha kilimo cha wananchi wa Mkoa wa Iringa na kufanya kiwe cha tija na kuinua maisha ya wananchi wa mkoa huu, hivyo mkiwa kama wadau wakubwa wa kilimo tunategemea mtatusapoti katika kutimiza azma hii,”amesema Sendiga.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Biashara wa Yara, Andrew Ndundulu ametoa rai kwa wasambazaji wote wa bidhaa zao kuchangamkia fursa mbalimbali zanazopatikana ndani ya programu hiyo kwa kujisajili kwa wingi ili waweze kupata ponti ili kunufaika kwa kupata zawadi mbalimbali huku wakipata elimu ya utaalamu wa kilimo, hivyo kuweza kuwasaidia wakulima wanaokwenda kwao kununua bidhaa za Yara.

“Tunaahidi kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na uongozi wa Mkoa wa Iringa na pia tutaendela kubuni mbinu nyingine za kidijitali zaidi ili kuhakikisha wadau wetu wanapata mafanikio mengi zaidi katika kilimo,”amesema.