April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KDCU yaongeza tija ya uzalishaji wa Kahawa

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Karagwe

CHAMA cha Ushirika cha Wilaya za Karagwe na Kyerwa (KDCU) kimeongeza tija ya uzalishaji wa zao la Kahawa kufuatia kupata soko la uhakika la kimataifa la kahawa inayozalishwa kwenye Wilaya hizo Mkoani Kagera.

Meneja Mkuu wa KDCU, Oscar Mujuni ameuambia Mtandao huu kuwa, kuongezeka kwa tija na soko la kimataifa kwa zao la kahawa kutoka kwenye Wilaya hizo kumeongezeka baada ya kufanyika kwa marekebisho mbalimbali kwenye mchakato mzima wa kilimo unaozingatia ubora wa kahawa inayozalishwa.

Amesema, wamefanikiwa kupata wanunuzi hao kufuatia uamuzi wa kuzingatia ubora wa zao hilo hali iliyongeza imani ya wanunuzi wa kahawa duniani ambao sasa wanaagiza kiasi kikubwa zaidi cha kahawa kutoka Tanzania.

“KDCU imefanikiwa kupata wanunuzi wa kahawa kutoka nchi za Ulaya ikiwemo, Uswizi, Uingereza na Ufaransa hali inayoongeza tija ya uzalishaji kwa wanachama wa ushirika,” amesema Mujuni.

Uzalishaji na uchakataji wa zao la kahawa Mkoani Kagera umepunguza kwa kiasi kikubwa ukosefu wa ajira kwa kuongeza idadi kubwa ya maelfu ya watu wanaojiajiri au kuajiriwa kwenye kilimo cha zao hilo wakiwemo vijana, akina mama na hata wazee hali ambayo imewaongezea kipato na kuinua kiwango cha mahitaji yao.

“Uboreshaji wa sasa wa zao la kahawa ni bora zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma hasa kwa mwaka 2017 wakati ambao kahawa iliyozalishwa iliuzwa na maganda yake ikiwa haina thamani kubwa huku ikiwa inauzwa kwa mtu yeyote yule huku kukiwa hakuna taarifa za ziada endapo kahawa ilikuwa inafika kwenye soko la kahawa la kimataifa,”.

“Lakini mfumo wa sasa wa ushirika unaongeza thamani ya kahawa inayokusanywa kutoka kwa mkulima na kufikishwa viwandani ili kukobolewa na kupangwa kwenye madaraja mbalimbali hali inayowezesha kahawa hiyo inayozalishwa kwenye Wilaya za Karagwe na Kyerwa kufika kwenye masoko ya kimataifa yakiwemo yale ya London, Uingereza na New York, Marekani,” amesema Mujuni.

Amesema, hatua ya uongezaji wa thamani kwenye zao la kahawa imempa mkulima uhakika kuwa kahawa anayoiuza itanunuliwa kwa bei iliyo kwenye soko la dunia kuliko ilivyokuwa hapo awali pale kahawa ilipokuwa ikiuzwa ngazi yoyote ile isiyo na tija kwenye bei.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na KDCU, unaonesha kuwa Wilaya za Karagwe na Kyerwa ambazo kupitia Chama Kikuu cha KDCU kinachozihudumia Wilaya hizo mbili kwa pamoja kupitia vyama vyama vyake vya msingi vya ushirika vipatavyo 125, zimeongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo kwa kiasi kikubwa hasa kwenye msimu wa zao hilo mwaka 2019/2020 hadi msimu wa mwaka 2021.

“Kutokana na usimamizi ulioko kwenye vyama vya ushirika mkulima amewezeshwa sasa kutambua umuhimu wa kuuza kahawa yake bila maganda ikiwa imekobolewa hali inayoinua thamani ya kahawa na kuiongezea bei kwenye soko la kimataifa,” amesema Mujuni.