March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jumuiya ya Afrika Mashariki kutekeleza adhima ya kurasimisha biashara

Judith Ferdinand, Mwanza

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira Walemavu),Jenista Mhagama, amesema serikali zote katika Jumuiya ya Afrika Mashariki,zinaendelea kutekeleza adhima ya kurasimisha biashara kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali.

Mhagama amesema hayo wakati akizungumza Kwenye siku ya Tanzania katika maonesho ya 21 ya wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali,Nguvu kazi yanayofanyika uwanja wa Rock City Mall mkoani Mwanza huku Tanzania ikiwa ni wenyeji wa maonesho hayo.

Amesema,uboreshaji wa mazingira ya biashara,bidhaa na huduma ambazo zimezalishwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kuzirasimisha biashara na bidhaa zao ni jambo la msingi.

Ambapo kwa mwaka huu Tanzania katika maonesho hayo wamejaribu kuweka mazingira rafiki kwenye mipaka yao ya kumuwezesha mjasiriamali.

“Sisi serikali zetu zote katika Afrika Mashariki,zinaendelea kutekeleza adhima ya kurasimisha biashara kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali,lakini uwepo wa huduma stahiki za usajili,vilevile miundombinu ya kuweza kufanya biashara zenu mkiwa salama,”amesema Mhagama.

Hivyo alitoa wito kwa wafanyabiashara Watanzania na wale wageni kutembelea mabanda ya taasisi zinazojishughulisha na utoaji huduma za kuwezesha urasimishaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini,ili kupata elimu itakayoweza kuwasaidia kukua kwa pamoja.

“Ndio maana maonesho haya sisi hapa Tanzania tumeamua kualika taasisi zile muhimu zinazoshughulika na utoaji wa huduma za kuwezesha urasimishaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi katika taifa letu,mmewaona hapa tunao TBS,NSSF,TMDA,TRA na taasisi nyingine nyingi, hivyo mkatembele katika mabanda yao ili mpate elimu,”.

Akizungumza maonesho hayo Mhagama amesema, yanawasaidia kutengeneza mshikamano mkubwa zaidi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia kufahamiana, kubadilishana ujuzi wa uzalishaji bidhaa kwenye sekta ya ujasiriamali ambao kesho yake wajasiriamali ndio watatengenezeana masoko kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.

“Ni jambo kubwa na ni chachu ya ukuaji wa uchumi na utatuzi wa ajira katika nchi zetu na kutoa fursa za ukuaji
wa biashara katika nchi zetu,”.

Sanjari na hayo amesema maonesho hayo yakiendelea kusimamiwa vizuri yanaweza kuondoa umaskini kwa kiasi kikubwa,hasa kufanya wajasiriamali wadogo waweze kukua na kumiliki viwanda vikubwa vya uzalishaji wa bidhaa hasa za asili ambazo zinapendwa sana katika masoko mengi katika ulimwengu mzima.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara na Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Keneth Bagamuhunda, amesema wajasiriamali ni sehemu kubwa ya kuunda sekta binafsi.

Bagamuhunda amesema,wameona maendeleo ya hayo maonesho kwani walianza na watu wachache lakini sasa namba imeongezeka,tofauti ya bidhaa imeongezeka,ubora wa bidhaa umeongezeka na kuunganisha watu kutoka muunganiko huo umeongezeka.

“Tunapaswa kuwaandaa wajasiriamali kuchukua fursa tulionayo kama Jumuiya ya Afrika Mashariki kuingia soko kuu,soko la pamoja la Afrika nzima,na wajasiriamali hawa waweze kuwa wakubwa,” amesema Bagamuhunda.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama(katikati) akishuhudia namna Mkurugenzi wa Biashara na Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Keneth Bagamuhunda( wa kwanza kushoto) akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake wa kuratibu vizuri maonesho ya 21 ya wajasiliamali ya EAC ya
Jua Kali,Nguvu kazi Mwenyekiti wa maandalizi ya maonesho hayo ambaye ni Mkurugenzi wa Ajira katika Wizara ambayo Mhagama anaiongoza Ali Msaki,katika siku ya Tanzania katika maonesho hayo yanayofanyika Mkoa Mwanza uwanja wa Rock City Mall.