April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sekta isiyo rasmi yachukua sehemu kubwa ya ukuzaji wa uchumi na uzalishaji wa bidhaa

Judith Ferdinand, Mwanza

IMEELEZWA kuwa sekta isiyo rasmi inachukua sehemu kubwa ya ukuzaji wa uchumi na uzalishaji wa bidhaa katika nchi nyingi hasa ambazo zinaendelea.

Ambapo mwaka huu wa 2021 Tanzania imekamilisha utafiti wa hali ya nguvu kazi na miongoni mwa matokeo ya utafiti huo ni kuwa na ongezeko la watu wanajishughulisha katika sekta isiyo rasmi kufikia asilimia 29.4 kwa mwaka 2020/21 toka asilimia 22.0 kwa mwaka 2014.

Akizungumza Kwenye siku ya Tanzania katika maonesho ya 21 ya wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali,Nguvu Moja yanayofanyika uwanja wa Rock City Mall mkoani Mwanza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira Walemavu),Jenista Mhagama, amesema wanaamini sekta hiyo kadri inavyoendelea kukua itatoa mchango mkubwa katika maendeleo na uchumi wa taifa.

Mhagama, amesema Mwaka huu wa 2021 nchi imekamilisha utafiti wa hali ya nguvu kazi na katika kufanya utafiti wa hali ya nguvu kazi matokeo yapo maeneo katika utafiti huo yamejionesha dhahiri kuwa taifa lina ongezeko la nguvu kazi ya watu takribani milioni 3.7 katika kipindi cha miaka 6 iliyopita kutoka watu milioni 22.9 kwa mwaka 2014 na sasa nguvu kazi imefika milioni 26.6 kwa mwaka 2020/21.

“Lakini la kufurahisha utafiti huo unaonesha kuwa watu wanajishughulisha katika sekta isiyo rasmi wameongezeka kufikia asilimia 29.4 kwa mwaka 2020/21 kutoka asilimia 22.0 kwa mwaka 2014,”amesema Mhagama.

Pia amesema,kufanya biashara au shughuli za kiuchumi katika sekta isiyo rasmi ni daraja la kukufikisha sehemu ambayo kila mmoja anaihitaji na kila mmoja anatamani kukua atoke kwenye sekta isiyo rasmi haweze kufika kwenye sekta rasmi na awe mzalishaji mkubwa.

“Sekta yenu inakuwa sana,sasa ni sekta ambayo tunatakiwa tuitizame mmemuona Rais wa Jamhuri ya Tanzania anapozungumza habari ya wamachinga, wajasiriamali wadogo anajua nini anachotaka kukifanya,anajua kwa ukuaji wa sekta hii ambao unatokana na matokeo ya utafiti,liko jambo lake kubwa kwenye sekta hii ili kukuza uchumi wa taifa letu,”amesema Mhagama.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel alitoa salamu za Mkoa, amesema kupitia maonesho hayo wanamwanza wanapata fursa ya kujifunza kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na kudumisha undugu.

Mhandisi Gabriel, amesema wajasiriamali kutumia fursa hiyo kubadilishana uzoefu na kuimarisha mahusiano ya biashara hasa kipindi ambacho kutakuwa hakuna maonesho.

Ameomba Mkoa wa Mwanza upewe hadhi yà kuandaa maonesho hayo mwakani,kwani ni mkoa huo ndio katikati ya nchi za Afrika Mashariki na unafikika kwa urahisi.

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wa Mwanza na maeneo jirani kujitokeza na kutembelea mabanda katika maonesho na kununua bidhaa mbalimbali.

“Tumepita kwenye mabanda tumeona bidhaa nyingi nzuri,wananchi tembeleeni katika maonesho haya kwani mkitaka bidhaa kwa ajili ya mwaka mpya na Christmas zipo hapa kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki,hakuna kiingilio ni bure,”amesema Mhandisi Gabriel.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge, Kazi, Vijana, Ajira,Walemavu)Jenista Mhagama(watatu kutoka kushoto),akiwa ameshika nyoka wa kikundi cha ngoma Bujora,wakati kikundi hicho kikitoa burudani katika siku ya Tanzania katika maonesho ya 21 ya wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali,Nguvu Moja yanayofanyika katika uwanja wa Rock City Mall mkoani Mwanza,huku pembeni yake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel.picha na Judith Ferdinand.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge, Kazi, Vijana, Ajira,Walemavu)Jenista Mhagama, akizungumza katika siku ya Tanzania katika maonesho ya 21 ya wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali,Nguvu Moja yanayofanyika katika uwanja wa Rock City Mall mkoani Mwanza,picha na Judith Ferdinand.