Mwandishi: Ismail Mayumba
Kujua eneo ambalo simu yako ipo wakati hujaishika au haipo karibu nawe ni jambo muhimu sana katika kulinda usalama wa kifaa chako na taarifa zako binafsi. Katika zama hizi za teknolojia, kuna njia mbalimbali zinazoweza kukusaidia kufuatilia simu yako, lakini mojawapo ya njia rahisi na inayotumika sana ni kupitia akaunti yako ya Gmail.
Ili uweze kutumia njia hii, jambo la kwanza kabisa ni kuwa na akaunti ya Gmail. Baada ya hapo, ni muhimu kuhakikisha kuwa simu yako imeunganishwa na akaunti hiyo ya Gmail. Hii ina maana kuwa lazima uwe umeingia (logged in) kwenye akaunti yako ya Google ndani ya simu husika. Hatua hii ni ya msingi kwa sababu ndiyo inayoruhusu huduma za Google kutambua na kufuatilia kifaa chako.
Baada ya kuhakikisha hayo, unaweza kufungua kivinjari (browser) kwenye simu nyingine, kompyuta au laptop, kisha uandike maneno “Find My Phone” au uende moja kwa moja kwenye huduma ya Google inayohusika na kutafuta vifaa vilivyopotea. Utahitajika kuingia kwenye akaunti yako ya Gmail ili kuthibitisha kuwa wewe ndiye mmiliki halali wa simu hiyo. Mara tu unapoingia, utaweza kuona ramani inayoonyesha eneo ambalo simu yako ipo kwa wakati huo.
Mbali na kuonyesha eneo la simu, huduma hii pia hutoa taarifa muhimu kama vile namba ya utambulisho wa kifaa (IMEI), hali ya betri, na kama simu imeunganishwa na mtandao au la. Hii inaweza kusaidia sana katika kufanya maamuzi sahihi ya hatua za kuchukua.
Endapo simu yako imepotea, huduma hii inakupa chaguzi kadhaa muhimu. Kwanza, unaweza kuipigia simu yako (ring) hata kama ipo kwenye hali ya kimya, jambo ambalo linaweza kusaidia kuipata ikiwa ipo karibu. Pili, unaweza kuiweka katika hali ya “simu iliyopotea” (lost mode), ambapo unaweza kufunga simu ili mtu mwingine asiweze kufikia taarifa zako. Aidha, unaweza pia kufuta taarifa zote zilizopo kwenye simu ikiwa unaona kuna hatari ya taarifa zako kuangukia mikononi mwa watu wasiofaa
Ni muhimu kufahamu kuwa huduma hii inafanya kazi vizuri zaidi pale ambapo kipengele cha “location” (eneo) kimewashwa kwenye simu yako. Hivyo, unashauriwa kuhakikisha kuwa huduma ya location ipo wazi (imewashwa) muda wote ili kurahisisha ufuatiliaji wa simu yako endapo itapotea. Hata hivyo, hii pia ni changamoto kwa sababu baadhi ya wezi wana uelewa wa teknolojia na wanaweza kuzima huduma hiyo ili kuficha eneo halisi la simu.
Kwa ujumla, kutumia akaunti ya Gmail kufuatilia simu ni njia ya awali na rahisi ambayo kila mtumiaji wa simu janja anapaswa kuijua. Ikiwa njia hii haitatoa matokeo yaliyotarajiwa, basi kuna mbinu nyingine za ziada na za kitaalamu zaidi zinazoweza kutumika kufuatilia au kurejesha simu iliyopotea.

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT