April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JE!, UNAWEZA KU-TRACK SIMU KWA KUTUMIA IMEI NAMBA?

MWANDISHI: Ismail Mayumba

IMEI (INTERNATIONAL MOBILE EQUIPMENT IDENTITY) ni namba ya kipekee inayotolewa kwa kila kifaa cha mawasiliano kinachotumia mtandao wa simu. Namba hii huifanya simu yako itambulike tofauti na simu nyingine yoyote duniani. Kwa lugha rahisi, IMEI ni kama kitambulisho cha taifa cha simu, kinachoonyesha upekee wake. Ingawa zipo njia nyingine za kutambua vifaa vya kielektroniki, IMEI inachukuliwa kuwa na usahihi mkubwa zaidi kwa sababu huwekwa moja kwa moja ndani ya kifaa (hardcoded) na haiwezi kubadilishwa kirahisi kama ilivyo kwa taarifa nyingine.

Kwa kawaida, simu nyingi huwa na namba moja au mbili za IMEI kutegemeana na idadi ya sehemu za kuweka laini (SIM slots). Hivyo, kila slot ya laini huwa na IMEI yake. Hii ina maana kuwa hata kama unatumia laini mbili kwenye simu moja, kifaa hicho bado kinaweza kutambulika kwa namba hizo za IMEI.

Umaarufu wa IMEI umeongezeka sana katika jamii baada ya watu wengi kuamini kuwa namba hiyo inaweza kusaidia kujua mahali simu ilipo pindi inapopotea au kuibiwa. Mara nyingi, mtu anapopoteza simu hukimbilia kwa wataalamu wa usalama wa mtandaoni au watu wanaodai kuwa wana uwezo wa kufuatilia simu kwa kutumia IMEI. Wengi huamini kuwa ni jambo rahisi kumpata mmiliki wa simu kwa njia hiyo. Hata hivyo, hali huwa tofauti pale juhudi hizo zinaposhindikana, na wakati mwingine wataalamu hulaumiwa au kuonekana hawana ujuzi wa kutosha.

Ni kweli kuwa namba ya IMEI inaweza kusaidia katika ufuatiliaji wa simu iliyopotea, lakini si kila mtu ana mamlaka au uwezo wa kuitumia kwa madhumuni hayo. Zipo programu maalumu (software) zinazotumika kufuatilia simu kwa kutumia IMEI, lakini mara nyingi programu hizo hutumiwa na mamlaka husika pekee. Programu zinazopatikana kwa urahisi katika jamii kwa kawaida hutoa taarifa za jumla tu, kama vile nchi ambayo simu ipo au mtandao unaotumika, bila kuonesha eneo halisi ilipo simu. Hivyo, mtu anapopoteza simu na kutegemea msaada wa watu wa kawaida au wataalamu binafsi, anaweza kupata msaada mdogo au usio kamili.

Kwa upande mwingine, IMEI ni nyenzo muhimu sana inapowasilishwa kwa vyombo vya dola au taasisi zenye mamlaka ya kushughulikia masuala ya mawasiliano. Taasisi kama Polisi, mamlaka za mawasiliano na mitandao ya simu zina uwezo wa kushirikiana kufuatilia kifaa kilichopotea kwa kutumia IMEI. Kwa sasa, mamlaka ya moja kwa moja ya kufuatilia na kuchukua hatua za kisheria mara nyingi huwa mikononi mwa Jeshi la Polisi. Mtu anapotoa taarifa ya kupotea kwa simu pamoja na IMEI yake, huwasaidia sana maafisa kufanya uchunguzi kwa ufanisi zaidi na kuongeza uwezekano wa kuipata simu hiyo.

Ni muhimu pia kufahamu kuwa, ingawa wapo watu binafsi au wauzaji wa simu katika baadhi ya maeneo wanaodai kusaidia kufuatilia simu kwa kutumia IMEI, kisheria hawana mamlaka ya kufanya hivyo. Hivyo, njia salama na sahihi zaidi ni kufuata taratibu rasmi kwa kutoa taarifa katika vyombo vinavyotambulika kisheria.

Ili kujua namba ya IMEI ya simu yako, unaweza kupiga msimbo *#06# kwenye simu. Baada ya kuibonyeza, namba ya IMEI itaonekana moja kwa moja kwenye skrini. Ni vyema kuihifadhi namba hiyo mahali salama, kama vile kwenye daftari, barua pepe au sehemu ya kuhifadhi taarifa mtandaoni. Hatua hii itakuwa msaada mkubwa endapo simu itapotea au kuibiwa, kwani utaweza kuitoa kwa mamlaka husika kwa haraka.

Kwa ujumla, IMEI ni sehemu muhimu ya usalama wa kifaa chako cha mawasiliano. Ingawa si suluhisho la pekee la kuzuia au kurejesha simu iliyopotea, inabaki kuwa nyenzo muhimu katika mchakato wa uchunguzi na ufuatiliaji. Elimu juu ya matumizi na umuhimu wake inaweza kumsaidia mtumiaji kuwa makini zaidi, kuchukua tahadhari mapema, na kufuata njia sahihi za kisheria pindi tatizo linapotokea.