May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii washauriwa kuwapa nafasi wenye ulemavu kuonyesha uwezo walionao

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira online,Dodoma

NAIBU Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Ummy Nderiananga ameitaka jamii kuwapatia watu wenye ulemavu nafasi ya kuonyesha uwezo walionao katika kuleta maendeleo kwenye maeneo yanayowazunguka.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Ummy Nderiananga akizungumza wakati alipofungua Kongamano la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanafunzi wenye Ulemavu na Maendeleo lililokuwa na kauli mbiu isemayo “Ulemavu si Kukosa Uwezo” kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Jijini Dodoma.

Ameeleza hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanafunzi wenye Ulemavu na Maendeleo lililokuwa na kauli mbiu isemayo “Ulemavu si Kukosa Uwezo.”

Kiongozi wa Wanafunzi wenye Ulemavu Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bw. Kelvin Mkude akisoma risala wakati wa kongamano hilo lililowakutanisha kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanafunzi wenye Ulemavu na Maendeleo lililokuwa na kauli mbiu isemayo “Ulemavu si Kukosa Uwezo” kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jijini Dodoma

Ameeleza kuwa Sera ya Taifa ya maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu yam waka 2004, Sheria ya Watu wenye ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 na Mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu 2006 imeeleza suala la ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli mbalimbali ikiwemo elimu, siasa, shughuli za uzalishaji mali, michezo pamoja na utamaduni.

Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (hayupo pichani) wakati wa Kongamano la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanafunzi wenye Ulemavu na Maendeleo lililofanyika katika chuo Kikuu cha Dodoma.

“Watu wenye Ulemavu wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa weledi na kwa ufanisi pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo endapo watapewa fursa na kushirikishwa kikamilifu, hivyo ni juku letu sote kuendelea kuelimisha jamii kuondokana na fikra potofu juu ya Watu wenye Ulemavu” amesema Naibu Waziri Ummy

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali na kwa kutambua uwezo mkubwa wa utendaji kazi waliokuwa nao wenye ulemavu.

“Kwa kutambua uwezo mkubwa waliokuwa nao watu wenye ulemavu Mheshimiwa Rais amefanya teuzi mbalimbali za uongozi kwa watu wenye ulemavu na hivyo ushirikishwaji pamoja na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo imekuwa ikiimarika siku hadi siku,” ameeleza.

Amefafanua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu shughuli za Watu wenye Ulemavu nchini kwa kuzingatia Sera,Sheria, Miongozo na Mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Taifa ya Mwaka 2030 na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Miaka Mitano 2021 – 2026.

Pia, ameeleza kuhusu utoaji wa mafunzo ya stadi za kazi na huduma za marekebisho kwa watu wenye ulemavu katika vyuo mbalimbali vinavyosimamiwa na Ofisi hiyo ikiwemo Chuo cha Yombo – Dar es Salaam, Sabasaba – Singida, Masiwani – Tanga, Luanzari – Tabora, Mirongo – Mwanza na Mtapika – Masasi pamoja na kuwashirikisha kikamilifu watu wenye ulemavu kwenye Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ummy ameelezea juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu na kujenga mazingira mazuri na fikivu ya kuwawezesha watu wenye ulemavu wanapata mahitaji yao kulingana na hali zao.

Sambamba na hayo ameupongeza uongozi wa chuo cha Dodoma (UDOM) kwa kuunda kitengo maalum kinachoshughulikia masuala ya Wanafunzi wenye Ulemavu pamoja na kuyapa kipaumbele mahitaji yao muhimu ya kielimu ikiwemo vifaa saidizi.