May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ETDCO:Mradi wa Umeme wa KV 33 Masasi–Newala wafikia asilimia 86 kukamilika

Na Penina Malundo,Timesmajira

Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme nchini (ETDCO), Mhandisi Richard Mwanja amesema mradi wa ujenzi wa njia ya umeme wa kilovoti 33 kutoka Masasi kwenda Newala umefikia asilimia 86 ya utekelezaji, huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Mei 20, 2026.

Amesmea ukamilikaji wa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza upatikanaji wa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Akizungumza leo Mei 8,2026 Mkoani Mtwara wilayani ya Masasi,Kaimu Meneja huyo ,Mhandisi Mwanja amesema mradi huo una urefu wa kilomita 76 na unahusisha ujenzi wa njia mpya ya umeme ambayo haijakatiza sehemu yoyote kutoka Masasi kuelekea Newala.

Amesema katika utekelezaji wa mradi huo jumla ya nguzo za zege 949 zinatakiwa kusimikwa, ambapo hadi sasa nguzo 914 tayari zimeshasimikwa.

“Huu ni mradi wa mwaka mmoja ambapo tuliingia site mwezi wa 10, hivyo tulitakiwa kumaliza mradi huu mwezi wa 10 mwaka huu,” amesema.

Aidha,Mwanja amesema kasi ya utekelezaji imeongezeka kutokana na ushirikiano na jitihada za viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mbunge wa eneo hilo Nawanda pamoja na maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Nishati chini ya Waziri wa Nishati.

“Kwasababu ya jitihada za viongozi wetu, sisi tunapambana kuhakikisha mradi huu unakamilika mapema, ndiyo maana ndani ya miezi saba tu tumefikia hatua kubwa ya utekelezaji,” amesema Mhandisi Mwanja .

Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuimarisha huduma ya umeme, kuchochea shughuli za kiuchumi pamoja na kuboresha maisha ya wananchi wa Masasi na Newala.