April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Emirate yachochea moto wa nyota Simba kimataifa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MORALI ya wachezaji wa klabu ya Simba katika mashindano ya Ligi Mabingwa Afrika sasa inatarajiwa kuwa juu zaidi baada ya Wadhamini wao kampuni ya Emirate Aluminium Profile kutangaza dau nono la Shh. Milioni 2.5 kwa mchezaji atakayechaguliwa kuwa nyota wa mchezo.

Katika michuano hiyo Simba imefanikiwa kutinga katika hatua ya robo fainali na kati ya Mei 14 na 16 watatupa karata yao ya kwanza dhidi ya wenyeji Kaizer Chief ya Afrika Kusini na watarudiana kati ya Mei 21 na 23 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Afisa Uhusiano wa Emirate Aluminium Profile, Issa Maeda amesema baada ya mchakato wa kutoa tuzo ya mchezaji bora wa klabu ya Simba kwenda vizuri sasa wameamua kwenda mbali zaidi na kuanza kutoa tuzo katika mechi za robo fainali za Ligi Mabingwa Afrika.

Hadi sasa tuzo hiyo iliyoanza kutolewa rasmi mwefi Februari imeshanyakuliwa na nyota watatu ambao ni Luis Miquissone, Machi ilikwenda kwa beki Joash Onyango lakini mwezi Aprili ikichukuliwa na kinara wa pasi za mwisho ‘Assist’ ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Clatous Chama.

Licha ya kuwa jambo hilo lipo nje ya mkataba, lakini walichokiangalia ni uzalendo kwani wanachokitaka ni kuongeza morali kwa wachezaji wa Simba kwani inapofanya vizuri basi inaitangaza vema nchi ya Tanzania na kufanya itamkwe vizuri nje ya mipaka.

“Tuzo hii ya nyota wa mchezo itakuwa tofauti na ile ya Mchezaji Bora wa Mwezi  hivyo mchezaji atakayechaguliwa kuwa nyota wa mchezo katika mkondo wa kwanza na wa pili  watachukua kitita cha Sh. Milioni 2.5,”.

“Ikiwa Simba itatinga nusu fainali katika michuano hiyo, basi tuzo hii itaendelea kwa kiashi cha milioni 2.5 katika kila mchezo ambazo zitafanya kuwa Sh. Milioni 10 ambazo tayari zimeshatengwa kwa ajili yao,” amesema Maenda.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo yake na Mchezaji Bora wa Aprili pamoja na kitita cha Sh. Milioni 1, Chama amesema kuwa, tuzo hiyo itazidi kuongeza morali kwa klabu ya Simba kwani sasa kila mchezaji atajituma ili kuweza kuipata.

“Tuzo hii ina maana kubwa kwangu kwani kama mnakumbuka sikuwa nimepata tuzo zaidi ya ile ya mchezaji Bora wa mwezi lakini mwisho wa msimu nikabeba tuzo ya Mchezaji bora wa msimu jambo ambalo lilikuwa zuri kwangu na kwa klabu, kwani imetufanya kama wachezaji kuwa na morali ili kuipa mafanikio timu yetu,” amesema Chama.

Nyota huyo amesema, kwa sasa jambo kubwa kwake na wenzake ni kuhakikisha timu yao inaendelea kufanya vizuri na kupata matokeo bora na tuzo hizo wanazichukulia kama sehemu ya kuwaongezea morali inayowasukuma, kuwatia moyo, kuwahamasisha kufikia malengo yao ikiwemo kutwaa taji la VPL, Kombe la Shirikisho pamoja na kufanya vizuri kwenye michuano ya kiamataifa.

Hivi karibuni nyota huyo wa Simba, aliweka wazi kuwa kwa sasa jambo kubwa kwake ni kuendelea kuitumikia klabu yake kwa ubora wa hali ya juu ili kuweza kuipa mafanikio wanayoyahitaji ikiwemo kuipambania nafasi ya ufungaji bora wa Ligi Mabingwa Afrika.

Hadi sasa katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi hiyo, Chama amefunga goli nne na kukaa kwenye nafasi ya tano katika orodha ya wafungaji bora wa michuano akizidiwa goli tatu na kinara Amir Sayoud wa CR Belouizdad mwenye goli saba huku Saifeldin Malik Bakhit wa Al Merrikh akiwa na goli sita.

Firas Chaouat wa Club Sportif Sfaxien ana goli tano huku Ayoub El Kaabi wa Wydad Casablanca, Chama na Mohammed Ali Ben Romdhane wa Esperence wakiwa na goli nne.

Sasa vita kubwa ipo kwa Sayoud, Kaabi, Chama na Romdhane ambao timu zao zimeshafanikiwa kutinga katika hatua ya robo fainali.

Ikiwa nyota huyo atafanikiwa kupata magoli katika mechi zao zijazo na Simba kusonga mbele zaidi basi atajiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwania kiatu hicho kwani hadi sasa baadhi ya washindani wake timu zao zimeshindwa kutinga robo fainali.

Mbali na Chama kuwania kiatu hicho nyota wa klabu ya Simba walioingia katika orodha ya wachezaji 150 waliofanikiwa kufunga katika michuano hiyo yupo Luis Miquissone aliyefunga goli tatu huku mshambuliaji Chris Mugalu akifunga goli mbili.