April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EAPCCO yajichimbia kujadili ugaidi

Martha Fatael, Timesmajira Online,Moshi

ZAIDI ya Askari 560 kutoka Shirikisho la Wakuu wa Polisi katika Nchi za Afrika Mashariki,(EAPCCO) wamejichimbia kwa siku sita Mjini Moshi, kujadili Ugaidi na namna fedha zinavyopatikana kufadhili matukio hayo.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Kazi amesema hayo wakati anafungua mafumzo ya mazoezi ya usalama pamoja yanayofanyika kwa vitendo na nadharia katika shule ya Polisi Moshi.

Amesema matukio ya ugaidi yanahitaji fedha nyingi na kwamba uchunguzi wa awali umebaini kuwa baadhi ya fedha hizo zinatokana na usafirishaji haramu wa binadamu, rushwa, dawa za kulevya na uhalifu mwingine unaovuka mipaka ya nchi.

“Tunayo timu ya wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi ambao watawafundisha Askari wetu namna ya kuchunguza, udhibiti na kufahamu upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufadhili matukio ya kigaidi,”amesema.

Amesema pamoja na masuala ya ugaidi na wizi wa kimtandao lakini pia Askari na maofisa hao watajadili na kuweka mikakati ya kudhibiti baadhi ya mianya inayohatarisha usalama baina ya nchi moja na nyingine.

Dkt. Kazi amesema mafunzo yanayotolewa yatawapa Askari hao utayari wa kupambana na matukio hayo wakati wowote yanapotokea na kuweza kuyadhibiti katika nchi hizo.

Awali Mkuu wa Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura amesema Tanzania inaunga mkono jitihada zinazofanywa katika kuhakikisha wanapambana na uhalifu unaovuka mipaka.