April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BoT kurejesha nidhamu ya fedha

Na Irene Clemence, Timesmajira Online,Dar

BENKI Kuu ya Tanzania(BoT) imedhamiria kutoa elimu ya fedha kuanzia ngazi ya elimu msingi hadi vyuo vikuu ili kuwapa uwezo vijana kuitawala fedha .
na sio iwatawale.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam Aprili 17, 2024 na Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga wakati akifungua warsha kuhusu uchopekaji wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu iliyowakutanisha viongozi mbalimbali na taasisi na elimu ya juu nchini.

Amesema BoT, itaendelea kusimama na vyuo na taasisi za elimu na Wizara ya Elimu katika kuhakikisha dhana ya elimu hiyo inakuwa endelevu na inafundishwa katika ngazi za jamii hata katika elimu zisizo rasmi.

“Wizara tutahakikisha elimu ya fedha inafundishwa katika mfumo wa elimu nchini hivyo twende kwa haraka kuhakikisha vijana ambao ni sehemu ya jamii nchini wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha hivyo natarajia wakuu wa vyuo mtabeba uelewa huo muhimu kwa vyuo vyetu nchini,” amesema.

Aidha aliviagiza vyuo vikuu kushirikiana na BoT kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango huo ili kuboresha mbinu na nyenzo za kufikisha ujumbe huo kwa jamii.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipatiwe taarifa ya tathmnini mtakazofanya ili itusaidie katika kufanya maamuzi, serikali imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa jamii,” amesema.

Naye Naibu Gavana wa BoT, Sauda Msemo amesema elimu ya fedha inakuwa ni sehemu ya masomo yafundishwe ngazi zote na somo hilo liingizwe kwenye mfumo ya elimu msingi hadi vyuo vikuu.

“Aprili mwaka jana, BoT iliwashirikisha wakuu wa taasisi za elimu ya juu nchini, kwa uwakilishi wa wakuu wa vyuo vikuu pamoja na TCU na NACTIVET kwa lengo la kukubaliana juu ya adhima ya kufundisha somo la elimu ya fedha ngazi ya elimu ya juu nchini.

Sauda amesema takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 inaonesha takribani watu asilimia 34.5 ni vijana walio na umri kati ya miaka 15-35 hivyo ili kuleta tija na ufanisi katika masuala ya uchumi ujuzi na uzoefu wa masuala ya fedha ni moja ya sifa muhimu kufikia azma hiyo.

Kwa upande wake, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA), Felix Adam amesema warsha hiyo ni muhimu kwake kwa sababu hayo maeneo yanayojadiliwa yatawasaidia kuwapa elimu ya fedha wahitimu wao.

” Sisi SUA tuliona changamoto na tukaanza maandalizi ya mitaala yetu ya elimu na kubuni mambo kadhaa hivyo mafunzo hayo yatasaidia kwenda kuboresha mitaala yetu ikiwa kubadilisha tabia za wahitimu kufanya maamuzi ya matumizi na uwekaji wa akiba ya fedha,” amesema.