May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Biteko: Uchaguzi utaenda Salama, Rais Samia analiongoza vizuri jahazi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline Dodoma

WATANZANIA wametakiwa kuwa na amani kwa kuwa uchaguzi utakwenda vizuri kuliko wakati wowote na Serikali haina hofu yoyote, wanajua Rais Samia Suluhu Hassan analiongoza vyema jahazi, atalifikisha salama mwaloni

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, wakati akifungua mkutano wa kitaaluma wa 13 wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioanza jana.

“Tunafahamu nyakati za uchaguzi baadhi ya watu huwa na tamaa ya kuchezea taarifa na kusukuma habari ‘feki’ kupitia mitandao ya kijamii. Hapa ndipo nataka tushirikiane kwa karibu ninyi wahariri na waandishi wa habari nchini, kuwafundisha hawa vijana na watu wanaoifanya kazi hii kupitia mitandao bila kufahamu maadili ya uandishi wa habari,” amesema Rais Samia.

Biteko, ameelezea kufurahishwa kusikia kwamba kwa sasa hamna tatizo la uhuru wa vyombo vya habari, hivyo alishauri kwa pamoja kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan aliyeboresha uhuru wa vyombo vya habari nchini na kuwapa mazingira bora ya kufanya kazi waandishi wa habari.

“Naamini tunapaswa kuungana sote kumpogeza Rais wetu kwa kuweka mazingira bora ya waandishi wa habari kufanya kazi na kwa pamoja tuseme asante,” amesema Biteko na kuongeza;.

Serikali ina imani ninyi wahariri na waandishi wa habari mtapima kwa haki utendaji wa Serikali iliyopo madarakani, mtapima ahadi zinazotolewa na kila upande na uwezekano wa kuzitekeleza, kisha muwasilishe kwa Watanzania nao wapime na kufanya uchaguzi sahihi kwa maendeleo endelevu ya taifa lao. Bila shaka chama kilichofanya vizuri kinafahamika na kitaendelea kufahamika.”

Kuhusu Dunia kumchagua Rais Samia kuwa Kinara wa uhamasishaji matumizi ya Nishati safi ya kupikia, ambayo ni gesi kwa Bara la Afrika, Dkt. Biteko alisema zipo faida nyingi unapotumia gesi, ambazo kati yake kubwa ni ulinzi wa misitu yetu na hivyo kuliepusha taifa na dunia na hatari ya jangwa.

“Tunapokata misitu, tunaharibu ardhi. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 16 ya ardhi ya nchi yetu imeharibiwa kutokana na ukataji miti holela,” amesema na kuongeza kwamba Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini ya Mwaka 2019, inaonesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 huharibiwa kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.

Hadi kufikia 2015, uzalishaji wa mkaa duniani ulikadiriwa kuwa tani milioni 52 kwa mwaka, na kati ya hizo tani milioni 32.4 zinazalishwa Afrika, ambapo asilimia 42 ya tani hizo zinazalishwa katika ukanda wa Afrika Mashariki unaohusisha nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi.

Afrika Magharibi inazalisha asilimia 32, Afrika ya Kati (12.2), Kaskazini (9.8) na Kusini mwa Afrika ni asilimia 3.4.

Takwimu hizi zinaashiria hatari kubwa. Misitu inateketea katika ukanda wetu. Wahariri fanyeni jambo. Ungeni mkono juhudi za serikali, vinginevyo kama tusipofanya kitu, nchi yetu itageuka jangwa si muda mrefu na kwa hakika sisi kama Serikali, hatutakubali hili litokee.

Katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG) ya Mwaka 2030, Lengo Na. 7 linaelekeza upatikanaji wa nishati safi na ya bei nafuu. Sisi hapa Tanzania tumebahatika kuwa na gesi ya kutosha. Ndiyo maana Mhe. Rais Samia amesema tuitumie gesi hii, ambayo ina bei nafuu tuokoe misitu na maisha ya kina mama huko vijijini.

Hili la kutumia gesi kama nishati ya kuendeshea magari, sisi kama Wizara tunalipa msukumo mkubwa. Tunajipnaga kujenga vituo vikukbwa vya kusambaza gesi ya magari na Kanuni imeruhusu sasa wenye vituo vya mafuta vya kawaida kuongeza uuzaji wa gesi, hii tukiamini itasaidia kuongeza kasi ya kusambaza gesi ya magari nchini.