May 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ahadi ya Rais Samia ya kumaliza mgao wa umeme nchini yatimizwa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetimizwa kwani kwa sasa hakuna mgao wa umeme.

Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo juzi wakati akifungua maonesho ya Wiki ya Nishati katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma, ambapo alimshukuru Rais, Dkt. Samia kwa kuimarisha Sekta ya Nishati kutokana na nyenzo na maelekezo anayoyatoa, ambayo yamempambanua kama kiongozi anayetatua matatizo ya wananchi kwa kutenda zaidi na si kusema.

“Nampongeza Rais Samia kwa kutimiza ahadi yake ya uwepo wa umeme wa uhakika nchini, kwani suala hilo sasa limeonekana kwa vitendo na malalamiko ya wananchi kuhusu changamoto za umeme
yamepungua na pia kwa nia dhati ya kuamua kumtua mama kuni kichwani kwa kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia,” amesema.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishat, Dkt. Doto
Biteko, akizungumza wataalam wa Taasisi mbalimbali
zilizo chini ya Wizara ya Nishat wakati wa ufunguzi wa
Maonesho ya Wiki ya Nisha 2024 katika Viwanja vya
Bunge jijini Dodoma Machi 16, 2024. Pamoja naye
ni Naibu Spika, Mussa Zungu

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, maelekezo ya Rais, Dkt. Samia pamoja na nyenzo anazozitoa kwa Wizara ya Nishati zimepelekea nchi sasa kuwa na umeme wa kutosha na kwamba hakuna mgawo tena, huku kukiwa na mitambo ambayo ipo tayari kuwashwa pale inapotokea hitilafu kwenye mitambo mingine ya uzalishaji umeme.

Aidha, kwa mikoa ambayo ipo nje ya gridi ya Taifa ikiwemo Katavi,
Rukwa, Kigoma, Lindi na Mtwara, alisema kuwa yote itaunganishwa kwenye gridi ya Taifa, kwani Rais, Dkt. Samia ameshatoa fedha za kutekeleza miradi ya umeme itakayoiunganisha mikoa hiyo na gridi ambayo tayari inaendelea.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kuimarisha utendaji kazi wao ikiwemo utatuzi wa changamoto za umeme akitolea mfano athari iliyotokea katika gridi ya umeme usiku wa siku ya Pasaka kutokana na hitilafu kwenye mfumo wa kudhibiti kiwango cha maji kwenye mitambo ya Kidatu, ambapo tatizo hilo lilipaswa kushughulikiwa kwa siku tatu, lakini TANESCO ilifanya jitihada na kutatua changamoto hiyo kwa muda wa saa kadhaa.

Pamoja na pongezi hizo Dkt. Biteko ametoa angalizo kwa kampuni tanzu za TANESCO kuhusu utendaji kazi wao ikiwemo Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) ambapo kampuni hiyo ilitoa ahadi ya kuanza uchorongaji wa visima vya Jotoardhi katika eneo la Ngozi Mbeya Aprili 1, 2024 lakini bado hawajaanza kazi hiyo.

Amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kuisimamia ipasavyo kampuni hiyo ili nchi iweze kupata umeme wa Jeothemo.

Pamoja na uendelezaji wa Sekta ya Umeme, Dkt. Biteko alisema kuwa
Wizara inaendelea na utekelezaji wa mipango mingine ikiwemo wa nishati safi ya kupikia ambapo Baraza la Mawaziri limeshapitisha Mpango Mkakati wa Nishati safi ya kupikia na sasa kinachofanyika ni utekelezaji ili asilimia 80 ya wananchi watumie nishati safi ya
kupikia ifikapo mwaka 2033.

Katika Sekta ndogo ya Gesi Asilia alisema kuwa, usimamizi madhubuti unaendelea ambapo chini ya Serikali ya Awamu ua Sita, imetolewa leseni ya uchimbaji wa Gesi asilia katika kisima cha Ntorya mkoani Mtwara, huku leseni ya mwisho ikiwa imetolewa mwaka 2006.

Kuhusu Maonesho ya Wiki ya Nishati, Dkt. Biteko amewaagiza Wataalam kuwa, pamoja na kueleza utekelezaji wa mipango ya Serikali na mipango mipya iliyopo lakini wanapaswa kutatua na kujibu hoja mbalimbali za wananchi na Wabunge na si kuzichukua ili kuyapa thamani maonesho hayo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nisha, Dkt. Doto
Biteko akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya
Wiki ya Nishati 2024 katika Viwanja vya Bunge jijini
Dodoma Machi 16 , 2024.

Vilevile, aliwapongeza Wabunge wote kwa usimamizi wa karibu wa Sekta ya Nishati na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na utatuzi wa kero zinazowahusu wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge. Mhe. Mussa Zungu amepongeza
Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa Maonesho hayo hususan matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kuhifadhi taarifa mbalimbali ikiwemo taarifa za maeneo yenye umeme, yasiyo na umeme, mfumo wa gridi n.k, suala linalowezesha taarifa hizo kupatikana kwa urahisi na kwa haraka pale zinapohitajika.

Ameeleza kuwa, Bunge litaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali na kuhakikisha fedha za kutekeleza miradi mbalimbali zinapatikana .