March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mwinyi atoa agizo kwa vyama vya michezo akipokea fedha za Mlandege

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha Vyama vya Michezo vinakuwa na utaratibu maalum utakaowezesha wafanyabaishara kujitokeza na kudhamini michezo hiyo.

Dkt. Mwinyi ametoa wito huo Ikulu Jijini Zanzibar, katika hafla ya makabidhiano ya
jumla ya Dola za Kimarekani 34, 000 ambazo ni zaidi ya Sh. milioni 78 zilizotolewa na Wafanyabiashara watano wa Zanzibar kwa ajili ya ushiriki wa timu ya Mlandege, kuelekea kwenye mchezo wao wa marudiano dhidi ya timu ya CS Sfaxien ya Tunisia ambao waliwafunga goli 5-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa visiwani humo.

Amesema, maendeleo ya michezo hapa nchini yatafikiwa kwa kuwepo udhamini wa uhakika utakaozinufaisha pande zote mbili kati ya wafanyabaishara na klabu huku akiwataka wafanyabiashara kote nchini kujitokeza kusaidia maendeleeo ya michezo, ikiwemo soka ili kurejesha hadhi ya mchezo huo iliyopotea.

Amesema kwa njia yoyote ile Taifa lina dhima ya kuhakikisha michezo inaimarika na kubainisha kuwa kamwe jambo hilo haliwezi kufikiwa bila ya kuwepo ufadhili ambapo Makampuni kwa utaratibu maalum yataweka fedha katika bajeti zao.

Pia amesitiza umuhimu wa Wizara hiyo kusimamia mashindano mbalimbali, akisema jambo hilo lina faida kubwa katika maendeleo ya michezo kwa kigezo kuwa huongeza hamasa, kuinua kipato pamoja na kukuza utalii nchini na kuagiza Wizara hiyo kuendelea na juhudi za kutengeneza viwanja kila mahali ili kuondokana na utaratibu wa timu kupokezana viwanja.

Dkt. Mwinyi amesema, azma ya vyama vya michezo kukaa na wadau ili kujenga mashirikiano na maelewano kati ya vyama vya michezo na klabu pamoja na wadau kwa ujumla.

Hivi sasa maelewano kati ya Viongozi wa ZFF na klabu za Unguja na Pemba hayako sawa, sambamba na kuwepo tatizo kubwa la ukosefu wa fedha za kuendeshea mashindano.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Mwita Maulid ameahidi kukaa na wadau ili kuimarisha maendeleo ya michezo nchini pamoja na maandalizi ya kufanikisha Kombe la Mapinduzi la 2021, kwa dhamira ya kurejesha hamasa na imani kwa wananchi.

Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Omar Hassan Omar ‘King’ aliishukuru Serikali kwa wito wake wa kuitaka Wizara hiyo kuwakutanisha na wadau wa michezo ili kufanikisha safari ya timu ya Mlendege kuelekea nchini Tunisia.

Pamoja na mambo mengine, akigusia kushuka kwa michezo nchini, amesema kwa kipindi kirefu Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na changmoto ya miundombinu ya michezo na ndio maana Chama cha Mapinduzi katika Ilani yake ikaazimia umuhimu wa kujenga viwanja katika Wialaya zote Unguja na Pemba.

Mfumo wa uendeshaji wa mpira wa miguu nchini nao uligubikwa na changamoto kubwa ya kuwa na idadi kubwa ya timu zinazoshiriki katika Ligi Kuu ya Zanzibar, jambo lisiloendana na maelekezo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kiongozi huyo amesema kuwa, kuwepo kwa timu 36 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar, hakuwezi kuwashajiisha wadhamini kuwekeza katika mpira hapa nchini kwani kuna changamoto ya mfumo wa kiutawala katika uendeshaji wa vyama vya michezo ikiwemo ZFF ambapo katiba yake inapswa kuwa na sifa zinazoendana na vyama vya soka vya nchi nyengine zilizo wanachama wa FIFA.

Wafanyabiashara waliofadhili fedha hizo wamesema, kuna umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha wadau wa michezo katika kila hatua ili kufanikisha maendeleo ya michezo nchini, ikiwemo soka uliopata umaarufu mkubwa hapa nchini katika miaka iliopita, umepoteza hadhi na hamasa kutokana an sababu mbali mbali, ikiwemo kutokuwepo ushirikishwaji wa wadau pamoja na mfumo mbaya wa uendeshaji.

Moja ya changamoto kubwa inayokwaza maendeleo ya soka nchini ni kwa Shirikisho la mchezo huo nchini (ZFF) kushindwa kukaa pamoja na klabu na kushirikiana katika masuala mbali mbali ya kuendeleza mchezo huo pamoja na utatuzi wa changamoto ziliopo.

Pia wameomba Serikali kuweka utaratibu mzuri wa matumizi ya viwanja vyake, ili kila timu iweze kupata fursa ya kuvitumia kwa mazoezi badala ya kuhodhiwa na timu maalum kama milki yake huku walieleza haja ya ZFF kuangalia uwezekano wa kubadili mfumo wa uendeshaji Ligi kwa timu za Vikosi kwa kuwa na timu moja, hatua itakayoziinua timu za kiraia ambazo ndio zenye mashabiki wengi.

Wamesema, ushiriki wa timu za kiraia, kama ilivyo sasa katika michuano ya ‘Ndondo na yamle yamle’ utaibua hamasa na kuleta ushindani mkubwa kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Wafanyabiashara hao pia wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na vyama vya michezo ili kuendeleza michezo mbalimbali nchini, wakibainisha hatua hiyo itawaweka vijana katika maadili mema na kuondokana na vitendo viovu, ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya.

Walimuomba Waziri anaehusika na michezo kuendelea kushirikiana nao na kubainisha utayari wao katika kusaidia maendeleo ya michezo mbali mbali nchini.

Aidha, akitoa shukrani, Mkurugenzi wa Klabu ya Mlandege Ali Khatibu Dai aliwashukuru wafanyabiashara hao kwa kujitolea kufanikisha safari ya timu hiyo kuelekea nchini Tunisia katika mchezo wao wa marudiano dhidi ya timu ya CS Sfaxien.

Amesema miongoni mwa athari kubwa ambayo Klabu ya Mlandege ingekabiliana nayo kwa kushindwa kushiriki katika mchezo huo wa marudiano ni kufungiwa na CAF, na hivyo kuliletea aibu Taifa.