July 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yazindua msimu wa sita Zanzibar Marathon 2026

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas Tanzania imezindua rasmi msimu wa sita wa mbio za Yas Zanzibar International Marathon 2026, ikiahidi kuendelea kuwekeza katika michezo, afya ya jamii na utalii wa michezo huku usajili wa washiriki ukifanyika kidijitali kupitia Mixx.

Yas ni mdhamini wa mashindano hayo kwa mwaka wa tano mfululizo na kwa mwaka huu mashindano yanatarajia kuvutia zaidi ya wakimbiaji elfu kumi (10,000) wa ndani nan je ya Tanzania, hatua inayolenga kuendelea kuitangaza Zanzibar kama moja ya nchi Kinara kwa utalii na michezo barani Afrika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Julai 23, 20266, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuendeleza matukio ya michezo yanayochochea uchumi, kukuza utalii na kuhamasisha wananchi kuishi maisha yenye afya.

“Yas Zanzibar International Marathon imeendelea kuwa zaidi ya mashindano ya riadha. Ni jukwaa linaloitangaza Zanzibar duniani, linakuza utalii wa michezo, linaibua vipaji na kuwahamasisha wananchi kuzingatia mazoezi kama sehemu ya maisha yenye afya.

“Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wanaowekeza katika maendeleo ya michezo na afya ya jamii,” amesema Dkt. Pembe.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, Innocent Rwetabura, amesema kampuni hiyo inaendelea kutumia michezo kama njia ya kuunganisha jamii, kuhamasisha mtindo wa maisha wenye afya na kuchochea ukuaji wa utalii wa michezo.
.
Amesema, ongezeko la washiriki wa marathon hiyo kila mwaka linaonyesha mwamko unaoongezeka wa Watanzania kuhusu umuhimu wa mazoezi, hasa katika kipindi ambacho taifa linaendelea kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

“Yas Zanzibar International Marathon imekuwa jukwaa muhimu linalowaunganisha watu kutoka ndani na nje ya Tanzania, kukuza vipaji vya vijana na kuitangaza Zanzibar kama kitovu cha utalii wa michezo.

“Kadri idadi ya washiriki na wageni inavyoongezeka, ndivyo fursa zinavyoongezeka kwa sekta ya utalii, wafanyabiashara na uchumi wa Zanzibar kwa ujumla,” amesema Rwetabura.

Ameongeza kuwa, usajili na malipo yote ya washiriki yatafanyika kidijitali kupitia Mixx, hatua inayolenga kurahisisha huduma na kuwapa washiriki uzoefu wa kisasa wenye viwango vya kimataifa.

Mbali na udhamini wa mbio hizo, alisema Yas inaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano Zanzibar kupitia huduma za Fiber pamoja na mtandao wa 4G na 5G ili kuendana na mahitaji ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Marathon ya mwaka huu itafanyika chini ya kaulimbiu ya “Kasi Swadakta kwa Viwango”, huku waandaaji wakiwahimiza Watanzania na washiriki kutoka mataifa mbalimbali kujisajili mapema kushiriki tukio hilo la kimataifa linalotarajiwa kuvutia maelfu ya wakimbiaji na watalii visiwani Zanzibar.