April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Majule ahoji mkakati wa Serikali kuvutia uwekezaji

Na Joyce Kasiki Timesmajita online, Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalum, Dkt. Neema Majule, amehoji Serikali kuhusu mpango wa kusajili wawekezaji wote nchini kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA) ili kuwa na kanzidata sahihi ya uwekezaji.
Akiuliza swali hilo bungeni, Dkt. Majule alitaka kufahamu mikakati ya Serikali katika kuhakikisha wawekezaji wote, wa ndani na nje ya nchi, wanasajiliwa rasmi ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga na kusimamia uchumi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, alisema TISEZA inaendelea kutekeleza jukumu la kusajili miradi ya uwekezaji kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, ikiwemo kiwango cha mtaji.
Alieleza kuwa hadi sasa, Serikali kupitia TISEZA imesajili jumla ya miradi ya uwekezaji 14,209 ambayo imepewa vyeti vya utambuzi.
“Mheshimiwa Spika, katika kuendana na maendeleo ya teknolojia ya kidigitali, TISEZA imekamilisha ujenzi wa Mfumo wa Kanzidata ya Taifa ya Uwekezaji wa Sekta Binafsi utakaounganisha mifumo ya taasisi mbalimbali zinazohusika na usajili wa makampuni ya wawekezaji nchini,” alisema Dkt. Chaya.
Aliongeza kuwa mfumo huo unalenga kuboresha upatikanaji wa takwimu sahihi za uwekezaji, hususan kuhusu mitaji iliyowekezwa na ajira zinazozalishwa na sekta binafsi.
Aidha, Serikali inaendelea na kampeni ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani kupitia wazawa, sambamba na kuwahamasisha wawekezaji ambao bado hawajasajiliwa kujitokeza ili kuingizwa kwenye mfumo rasmi.
Katika swali la nyongeza, Dkt. Majule alihoji kuhusu vigezo vinavyotumika kuwafanya wawekezaji wengi zaidi kujisajili pamoja na vivutio vinavyotolewa ili kuongeza idadi ya wawekezaji nchini.
Akijibu, Dkt. Chaya alifafanua kuwa kwa wawekezaji wazawa, kiwango cha chini cha mtaji ni dola za Marekani 50,000 (takriban shilingi milioni 125), huku kwa wawekezaji wa kimkakati wa ndani wakitakiwa kuwa na mtaji wa dola milioni 50.
Kwa upande wa wawekezaji wa nje, alisema wawekezaji wa kawaida wanatakiwa kuwa na mtaji usiopungua dola 500,000, wakati wawekezaji wa kimkakati wanapaswa kuwa na angalau dola milioni 500.
Kuhusu vivutio, Naibu Waziri alibainisha kuwa Serikali imeweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi ili kuwavutia wawekezaji zaidi kuwekeza nchini na kujisajili rasmi kupitia TISEZA huku akisema,hatua hiyo inaelezwa kuwa itasaidia kuongeza uwazi, ufuatiliaji na mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa.