Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuimarisha vitengo vya tathmini na ufuatiliaji katika kila wizara ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akijibu swali la Mbunge wa Monduli, Isack Copriano, katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni, aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali katika kuimarisha timu hizo ili kuharakisha utatuzi wa kero za wananchi, Dkt. Nchemba alisema vitengo hivyo vitawezeshwa kwa rasilimali za kutosha ili kuongeza ufanisi wake.
Katika swali lake,Mbunge huyo alieleza kuwa kutokana na ziara mbalimbali za Waziri Mkuu, amekuwa akipokea kero nyingi za wananchi ambapo baadhi hupatiwa majibu papo kwa papo, huku nyingine zikikosa majibu au kupelekwa kwenye timu ya tathmini na ufuatiliaji ambako majibu yake yamekuwa hafifu.
Alihoji ni mkakati gani wa Serikali wa kuimarisha timu hizo ili ziweze kuharakisha utoaji wa majibu kwa wananchi, hususan waishio vijijini.
Akijibu hoja hiyo, Dkt. Nchemba alisema Serikali inapanga kuongeza bajeti kwa vitengo hivyo ili viweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake, hususan katika kufuatilia utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha, alisema Serikali imeanzisha kituo cha kupokea simu (Call Centre) namba 190, kitakachowawezesha wananchi kuwasilisha kero zao na kupata majibu kwa wakati.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali inakusudia kurejesha utaratibu wa viongozi kutumia rejesta maalumu kurekodi na kufuatilia kero za wananchi, ambapo taarifa zitakuwa zinawasilishwa kila mwisho wa mwezi.
“Utaratibu wa kushughulikia kero za wananchi hautakuwa wa msimu au wa ziara pekee. Kila kiongozi atawajibika kutoa taarifa ya idadi ya wananchi aliowahudumia, majibu aliyotoa pamoja na hatua zilizochukuliwa kutatua changamoto zao,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi bila kulazimika kuwafuata viongozi, huku kero zao zikishughulikiwa kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT