April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madai wafanyakazi kiwanda cha Mgololo yatua Bungeni

Na Joyce Kasiki,Timemsjaira online,Dodoma

MBUNGE  wa Mafinga Mjini,  Dickson Lutevele, ameihoji serikali kuhusu kuchelewa kwa malipo ya madai ya wafanyakazi wa zamani wa Kiwanda cha Karatasi cha SPM Mgololo, akieleza kuwa wafanyakazi hao wamekaa muda mrefu wakisubiri haki yao bila mafanikio. 

Akiuliza swali la msingi leo Aprili 8,2026 bungeni jijini Dodoma, Lutevele alitaka kujua ni lini hasa serikali itatekeleza malipo hayo, akisisitiza kuwa madai hayo ni ya muda mrefu na yamewaathiri wahusika kwa kiasi kikubwa.

 Katika maswali yake ya nyongeza, ameeleza kuwa wafanyakazi hao walishinda kesi ya msingi mwaka 2007 ambapo mahakama iliamuru walipwe na pande zote mbili, yaani mwekezaji na serikali, na hivyo akahoji iwapo serikali haioni haja ya kumaliza mgogoro huo ili kuhakikisha wanapata haki yao kwa wakati. 

Aidha, amerejea kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuacha tabasamu kwa watanzania, akihoji kama serikali haioni umuhimu wa kuharakisha fidia kwa wafanyakazi hao ambao wameendelea kusubiri kwa muda mrefu huku wakikabiliwa na ugumu wa maisha.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara,  Dennis Londo, ameeleza kuwa madai hayo yanatokana na mchakato wa ubinafsishaji wa kiwanda hicho mwaka 2004, ambapo baadhi ya wafanyakazi walipunguzwa kazi.

 Amefafanua kuwa mwekezaji tayari alishalipa sehemu ya madai yanayomhusu, huku serikali ikiingia katika suala hilo kwa kuwa ndiyo iliyokuwa mmiliki wa awali kabla ya ubinafsishaji. 

Londo ameongeza kuwa serikali ilishawahi kutenga fedha kwa ajili ya kulipa madai hayo katika mwaka wa fedha 2017/2018, lakini baadhi ya wadai walikataa kupokea wakidai kiwango kilichotolewa kilikuwa kidogo. 

Hata hivyo, amesisitiza kuwa nia ya serikali ni kumaliza mgogoro huo kwa kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha wafanyakazi hao wanapata stahiki zao, huku akibainisha pia kuwa suala hilo bado lipo katika ngazi ya Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi.