April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko atoa maagizo Wizara ya maji

📌 Asisitiza Wananchi kutoa maoni utunzaji wa mazingira katika Dira 2050

📌 Ataka Bodi za Mabonde ya Maji/NEMC kudhibiti uchafuzi wa mazingira

📌 Uvunaji wa Maji ya Mvua wasisitizwa ngazi ya Kaya, Taasisi hadi Taifa

📌 Amtaja Rais Dkt. Samia kinara wa kumtua Mama ndoo kichwani

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameitaka Wizara ya Maji kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama ili kuendana na thamani halisi ya miundombinu ya maji iliyojengwa na Serikali kwa gharama kubwa ili kuwapa huduma wananchi kwa ufanisi.

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo Jijini Dodoma tarehe 22 Machi, 2024 wakati akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Maji Tanzania ambayo yameenda pamoja na Siku ya Maji Duniani.

Ameagiza Wizara na Mamlaka za Maji zijielekeze kwenye ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo mabwawa ya kuvuna maji ya mvua katika maeneo yasiyo na vyanzo vya maji vya uhakika na kusisitiza kuwa suala hilo lisisubiri rasilimali fedha ya kutosha bali waanze kutekeleza na rasimali zitaendekea kuja wakati utekelezaji umeshaanza.

Vilevile ametoa wito kwa mwananchi mmoja mmoja, Taasisi za Serikali, Binafsi, Madhehebu ya Dini na makundi mengine kuweka miundombinu ya kuvuna maji ya Mvua kwenye nyumba zao ili kuimarisha upatikanaji wa maji kutokana na mvua zinavyopatikana.

Akizungumzia hifadhi na utunzaji wa mazingira, Dkt. Biteko amewataka Wananchi wajitokeze kutoa maoni katika mkakati wa hifadhi vyanzo vya maji wakati huu Serikali ikiendelea na utayarishaji wa Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 ili suala la hifadhi za vyanzo vya maji lipewe kipaumbe kinachostahili.

Aidha ameagiza Bodi za Maji na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuongeza jitihada za kudhibiti uchafuzi wa mazingira na hata wawekezaji wanapokuja nchini lazima wazingatie utunzaji wa mazingira ili yasiathirike.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amezishukuru Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika Sekta ya Maji na kuwaasa kuendelea kukuza ushirikiano ili kuwasambazia wananchi maji kwani bado kuna kazi kubwa ya kuwapelekea wananchi Maji.

Vilevile ameitaka Wizara ya Maji kusimamia kikamilifu maeneo yote yenye vyanzo vya maji, kujengea uwezo wataalam wake katika kuandaa maandiko ya maji yatakayowezesha kupata fedha zaidi za mabadiliko ya tabia nchi zitakazosaidia kupata fedha za utunzaji wa mazingira na pia Sekta zinazohusiana na maji zishirikikine kwa karibu katika usimamizi na si kila mtu kuwa na sheria yake hali inayoleta ukinzani katika utendaji wa kazi.

Kuhusu mpango uliopo wa uhifadhi wa vidakio vya maji ambao gharama yake ya utekelezaji ni shilingi bilioni 875 ambazo zinapaswa kutoka Sekta mbalimbali, Dkt. Biteko ameagiza Wizara ya Maji kutenga fedha kwenye bajeti yake ili kuhakikisha kuwa mpango huo unatekelezeka.

Amesema vyanzo vingi vya maji vimeharibika na vingine vinaendelea kuvamiwa hivyo Siku ya kilele cha Wiki ya Maji kila mtu ajitathmini na kuchukua hatua kuhusu juhudi zinazowekwa kwenye utunzaji wa mazingira ili vizazi vinavyokuja vikute mazingira yaliyo salama.

“ Tafiti za maji za mwaka 2019 zinaonesha kuwa, kiasi cha maji kinachopatikana kwa mtu kwa mwaka kinaendelea kupungua siku hadi siku kutoka mita za ujazo 12,600 katika kipindi cha Uhuru hadi mita za ujzo 2,105 kwa mwaka 2022 hivyo tusipochukua hatua na jitihada za makusudi hali hii itaendelea kushuka kila mwaka kwa sababu maji yanaendelea kupungua katika vyanzo,” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kumtua mwanamke ndoo kichwani kwa kutenga fedha, kutoa maelekezo na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji nchini.

Awali, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema kuwa miaka ya nyuma Wizara hiyo ilikuwa ya kero na lawama lakini kutoka Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ameibadilisha na kuendelea kumtua mama ndoo kichwani na pia ametekeleza miradi mingi ambayo huko nyuma ilikwama.

Amesema katika Vijiji 12, 318 tayari vijiji 9,737 vimesambaziwa maji ambapo amewataka wataalam katika Wizara hiyo kutozoea shida za Wananchi hivyo popote pale ambapo maji yanahitajika basi wananchi wapate maji ikiwemo kuchimba visima vitakavyowasaidia wananchi kupata maji.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria Maadhimisho hayo ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Selemani Jafo na Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Joseph Kilangi.