July 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dereva wa John Heche afariki Kigoma, damu zatapakaa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kifo cha ghafla cha Suez Dani Maradufu, ambaye alikuwa dereva wa Makamu wa Mwenyekiti Bara, John Heche.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatano, Julai 01, 2026, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CHADEMA, Amani Golugwa, amesema marehemu amekutwa amefariki dunia asubuhi hii akiwa chumbani kwenye nyumba ya wageni mjini Kigoma.

“Kwa masikitiko makubwa tunathibitisha kuwa mwendazake Suez amekutwa akiwa amefariki na damu zimetapakaa sakafuni ndani ya chumba chake. Tukio hilo limetuacha na masikitiko makubwa sana,” amesema Golugwa.

Golugwa amebainisha kuwa mara baada ya taarifa hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma lilifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka hospitali ya mkoa wa Kigoma kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Huu ni msiba mzito kwa chama chetu na kwa familia ya Heche. Tumepigwa na butwaa kuondokewa na mtumishi mwaminifu. Tunatoa salamu zetu za dhati za pole kwa familia, wanachama, ndugu na marafiki,” amesema.

Golugwa amesema chama kitaendelea kutoa taarifa zaidi kadri uchunguzi wa Polisi utakavyoendelea.

Taarifa ya chama imehitimishwa kwa maneno, “Bwana alitoa. Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Amina.”