Na Joyce Kasiki
MTAFITI wa Afya ya Binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Ndaki ya Afya ya Sanyansi Shirikishi Mbeya (MCHAS) Dkt. Bernard Mbwele amesema utafiti unaolenga kuboresha huduma za uzazi umeonyesha umuhimu wa kuwapa wajawazito huduma zenye heshima, utu na mawasiliano mazuri ili kupunguza vifo na madhara yanayotokana na uzazi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Julai Mosi mwaka huu katika maonyesho ya Kinataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba ,Mtafiti huyo amesema amejikita zaidi katika tafiti za afya ya mama na mtoto kwa kuwa ni eneo linalogusa maisha ya kila binadamu.
Ameelleza kuwa licha ya Tanzania kuwa na wahudumu wenye ujuzi wa uzazi katika vituo vya afya, bado changamoto za mtazamo na namna ya kuwahudumia wajawazito zinaendelea kujitokeza.
Amesema wakati wa mafunzo yake ya udaktari alishuhudia baadhi ya wajawazito wakitendewa kwa lugha kali na vitendo visivyozingatia utu, jambo lililomsukuma kufanya utafiti kuhusu uzoefu wa wanawake wanapopata huduma za uzazi.
Kwa mujibu wake, matokeo ya utafiti yalibaini kuwa matukio ya huduma zisizo rafiki yamekuwa yakitokea katika baadhi ya vituo vya afya, hali inayoweza kusababisha wajawazito kuchelewa kufika hospitalini, kupata madhara ya kudumu au hata kupoteza maisha yao na watoto wao.
Kutokana na hali hiyo, timu ya watafiti ilianzisha mradi unaolenga kuboresha huduma zinazomweka mgonjwa katikati ya maamuzi ya matibabu (patient-centered care), kwa kuzingatia heshima, mawasiliano bora na ushirikishwaji wa mama katika huduma anazopokea.
Aidha, amesema walitafsiri na kuoanisha kwa lugha ya Kiswahili zana za kimataifa za kupima uzoefu na kiwango cha kuridhika kwa mama wakati wa kujifungua, mchakato ulioshirikisha wataalamu wa afya, wataalamu wa lugha kutoka Baraza la Kiswahili pamoja na wataalamu kutoka Marekani.
Ameeleza kuwa zana hizo zilitumika kufanya tathmini kwa makundi mbalimbali ya akina mama, ambapo ilibainika kuwa waliowahi kujifungua zaidi ya mara mbili walikuwa na uelewa mkubwa wa huduma kuliko wale waliokuwa wakijifungua kwa mara ya kwanza, hususan vijana wenye umri kati ya miaka 20 na 25.
Pia amesema utafiti ulionesha tofauti za ubora wa huduma kati ya baadhi ya hospitali, huku wanawake wa mijini wakionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuuliza maswali na kushiriki maamuzi kuhusu huduma za afya kuliko wale wa maeneo ya vijijini.
Kwa upande wa wanawake wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), amesema utafiti ulisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanapata huduma salama, zenye faragha na zisizo na ubaguzi ili kulinda afya ya mama na mtoto.
Mtafiti huyo alisema matokeo ya kazi hiyo yameanza kuchapishwa katika majarida ya kisayansi na kuvutia nchi mbalimbali za Afrika, huku baadhi zikitaka kutumia toleo la Kiswahili la zana hizo kwa tafiti na huduma za afya.
Ameongeza kuwa hatua inayofuata ni kushirikiana na Wizara ya Afya ili matokeo ya tafiti hiyo yawe sehemu ya sera na miongozo ya utoaji huduma za uzazi nchini.
Ametoa wito kwa wahudumu wa afya, familia na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kujenga mazingira ya huduma zenye heshima na utu kwa wajawazito, akisema kuboresha huduma za uzazi ni jukumu la kila mmoja na si la serikali pekee.
Amesema endapo hatua hizo zitatekelezwa kikamilifu, ndani ya miaka michache Tanzania inaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa vitendo vya ukatili na huduma zisizo rafiki kwa wanawake wakati wa kujifungua

More Stories
Tani 22.6 dawa za kulevya zakamatwa, 188 wanaswa
BRELA yaelekezwa kuwasaidia Wafanyabiashara maonesho ya Sabasaba
Serikali yaendelea kuboresha huduma usafi wa mazingira