Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline,Arusha
DIWANI wa Kata ya Mlangarini, Emanuel Mrema, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za awamu ya kwanza kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Manyire, mradi unaotarajiwa kuboresha upatikanaji wa elimu kwa wakazi wa eneo hilo.
Mrema ametoa shukrani hizo leo Julai 24,2026 ambapo amesema tayari mradi huo umekabidhiwa rasmi na hatua za awali za utekelezaji zimeanza, ambapo wananchi kwa kushirikiana na Mkandarasi wanaendelea na kazi ya kuchimba msingi wa majengo ya shule hiyo.
Amesema ujenzi wa shule hiyo ni faraja kubwa kwa wananchi wa Kijiji cha Manyire ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa shule ya sekondari karibu na makazi yao.
Kwa mujibu wa Mrema, wanafunzi wa eneo hilo walilazimika kutembea umbali wa hadi kilomita 24 kila siku kufuata masomo, hali iliyokuwa ikiathiri mahudhurio na maendeleo yao kitaaluma.
Ameeleza kuwa kufanikishwa kwa mradi huo kumetokana na juhudi za Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumayi, ambaye amekuwa akiwasilisha mara kwa mara bungeni hitaji la wananchi wa Manyire kupata shule ya sekondari.
Diwani huyo pia aliishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kupitia Mkurugenzi Mtendaji, Selemani Msumwi, kwa ushirikiano na juhudi zilizowezesha mradi huo kuanza kutekelezwa.
Aidha,amesema wananchi wa Manyire wanaendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na kuendelea kupeleka miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi.
Mrema amebainisha kuwa vijana wa Manyire ni wapenda maendeleo na tayari wamejitokeza kushiriki katika hatua za mwanzo za utekelezaji wa mradi huo, jambo linaloonyesha dhamira yao ya kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Amewataka wananchi wa Manyire kuendelea kushirikiana, kupenda maendeleo na kusimamia vizuri miradi ya Serikali ili iweze kudumu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
“Watoto wetu hawapaswi kurithi migogoro, matusi au visasi, bali wanapaswa kurithi miradi ya maendeleo ambayo itaboresha maisha yao na kuwapa fursa za kufikia ndoto zao,”amesema Mrema.

More Stories
Kampuni ya Oryx Gas yakabidhi mitumgi 600 kwa wajasiriamali
DCEA yafanikiwa kuteketeza ekari 291.2 Mara
Serikali yazindua mikopo nafuu kujenga vituo vidogo vijijini