November 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aibuka na fursa za dola bilioni 4.7 COP31

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

USHIRIKI wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 31 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) uliofanyika Antalya, nchini Uturuki, umeiwezesha Tanzania kupata ahadi za kifedha na fursa za uwekezaji zenye thamani ya takribani Dola za Marekani bilioni 4.7.

Ahadi hizo zinahusisha fedha kwa ajili ya nishati safi ya kupikia, uhifadhi wa mazingira, nishati jadidifu na miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimazingira nchini.

Akitoa taarifa ya matokeo na manufaa ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo,jijini Dar es Salaam mapema leo Novemba 27,2026 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, amesema ushiriki wa Rais Samia umeiwezesha nchi kupata mafanikio makubwa na kuendeleza vipaumbele vyake katika ajenda ya mabadiliko ya tabianchi.

Amesema miongoni mwa ahadi zilizopatikana ni Dola milioni 54 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kununua majiko 70,000 ya kisasa yanayotumia umeme kwa shule na vituo vya afya, pamoja na Dola milioni 26 kwa ajili ya kuhifadhi mifumo ikolojia ya pwani na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.

Aidha, Serikali ya Uingereza kupitia UK Aid imeahidi Pauni milioni mbili kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na Pauni milioni mbili nyingine kwa nishati jadidifu, huku ikisaidia wananchi milioni moja kupata majiko ya umeme kwa utaratibu wa kulipia gharama zake kidogo kidogo kupitia bili za umeme.

Masauni amesema taasisi ya SEforALL imeahidi kuijumuisha Tanzania katika nchi zitakazonufaika na uwekezaji wa zaidi ya Dola bilioni nne kwa ajili ya nishati safi ya kupikia, sambamba na kusaidia nchi kuwa kitovu cha uzalishaji wa majiko na teknolojia zinazohusiana na nishati hiyo.

Amesema kampuni ya UpEnergy imeahidi kuendeleza mradi wa nishati safi ya kupikia katika shule 3,000 za umma wenye thamani ya takribani Dola milioni 30 kupitia ushirikiano wa Tanzania na Japan katika biashara ya kaboni, huku Saudi Arabia ikiahidi kuendelea kufadhili miradi ya nishati jadidifu na nishati safi ya kupikia pamoja na kuunga mkono matumizi ya gesi asilia kama nishati ya mpito.

Katika hatua nyingine, amesema Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi umeahidi kuidhinisha miradi yenye thamani ya Dola milioni 40 kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), huku Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Kijani (GCF) ukiahidi Dola milioni sita kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa Tanzania kuandaa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Pia, Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu umeidhinisha mchakato wa kupata Dola milioni 20 kupitia CRDB Bank kwa ajili ya kusaidia jamii za visiwa vidogo, maeneo ya pwani na kanda za maziwa, hususan Pemba, Unguja, Kigoma na Pwani.

Ameongeza kuwa International Solar Alliance imeiweka Tanzania katika mpango wa Dola milioni 200, huku U.S.-China Green Fund ikiwa imeijumuisha nchi katika mpango wa Dola milioni 300 wa kusaidia mataifa yanayoendelea katika eneo la nishati safi ya kupikia.

Masauni amesema mafanikio hayo yanaambatana na hatua za kuimarisha uwezo wa Tanzania kunufaika na fedha za kimataifa, akibainisha kuwa GCF imetoa ithibati kwa NEMC na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache za Afrika zenye taasisi mbili zilizoidhinishwa kupata fedha za mfuko huo, ambazo ni NEMC na CRDB Bank.

AmesemaTanzania pia imesaini makubaliano ya ushirikiano na Sekretarieti ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) ili kuwa mwenyeji wa mikutano ya tabianchi, ikiwa ni nchi ya pili duniani kufanya hivyo.

Kupitia makubaliano hayo, amesema nchi inajiandaa kuwa mwenyeji wa mikutano miwili ya UNFCCC kuanzia Februari 2027, hatua inayotarajiwa kuimarisha diplomasia ya tabianchi na kukuza utalii wa mikutano.

Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) imesaini mikataba ya ushirikiano na taasisi za kimataifa za IETA, Evercity UG na Verra kwa ajili ya kujenga uwezo, kuimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni, usajili na uthibitishaji wa miradi pamoja na upatikanaji wa viwango vya kaboni vinavyokidhi viwango vya kimataifa.

Masauni amesema Tanzania pia imepata uthibitisho wa kuwa mwenyeji na kuanzisha Kituo cha Vijana Wajadili wa Tabianchi Afrika (Youth Negotiators Centre), kitakachojenga uwezo wa vijana kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Amesema Zanzibar nayo imenufaika baada ya kutunukiwa cheti cha kutambuliwa kama Jiji Linalosimamia Taka Vizuri (Zero Waste City) na kuchaguliwa kuwa miongoni mwa maeneo 20 ya awali katika nchi 11 duniani yatakayotekeleza Mpango wa Kimataifa wa Maeneo Yasiyo na Taka.

Akizungumzia utekelezaji wa ahadi hizo, Masauni amesema Serikali itafuatilia kwa karibu ahadi za kifedha na fursa za uwekezaji zilizopatikana ili kuhakikisha rasilimali hizo zinafika nchini na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Jukumu letu sasa ni kuhakikisha kuwa ahadi na fursa hizi zinafuatiliwa kwa karibu, taratibu zinakamilishwa na rasilimali zinageuzwa kuwa miradi na manufaa halisi kwa wananchi,” amesema

Amesema Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa matokeo ya COP31 kupitia wizara, idara na taasisi za Serikali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha fursa zilizopatikana zinachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.