May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo azitaka Tasisi zinazojihusisha na masuala ya ubunifu kuwasaidia wabunifu nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

KATIBU  Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM )Daniel Chongolo amezitaka taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya ubunifu  nchini ikiwemo Tume ya sayansi na teknolojia (COSTECH) pamoja na vyuo vikuu vinavyosimamia masuala ya uhandisi  (engineering) kuhakikisha wanasimamia mawazo ya ubunifu kutoka kwa wabunifu mbalimbali.

Pia ametoa siku saba kwa Shirika la Viwango nchini(TBS) kutembelea na kujiridhisha,ubunifu uliofanyika na Mbunifu Masoud Kipanya wa gari linalotumia umeme kwa kumpa ushauri wa kitaalamu na kama limelight vigezo vyote kumpatia namba ya ubora na kujisajili.

Chongolo alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea kiwanda cha kuunda gari inayotumia mfumo wa umeme nchini ya KP Motors  ambapo amewaasa Watanzania kujenga tabia ya kuwawezesha wabunifu kifedha na kuwapa moyo ili kuendeleza mawazo yao na kuleta matokeo chanya katika uchumi wa nchi. 

Alisema ni vema taasisi za serikali  zinazojihusisha na ubunifu na ufundi  kutoa msukumo na kuthamini mawazo ya wabunifu ili kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya nchi.

“Nmekuja kwaajili ya kutembelea kiwanda Cha Masoud kipanya ambapo niliona kwenye vyombo mbalimbali vya habari siku kadhaa zilizopita, ubunifu, uvumbuzi, ugunduzi uliotokana na wazo ambalo aliliwaza ndugu yetu na mwishoni ukatufanikishia kupata gari la kwanza linalotumia umeme Tanzania”alisema na kuongeza 

“Ndani ya siku 14 nitakuja tena na taaisisi zote za kiserikali na kila mmoja atoe maoni yake kwa eneo lake atasaidiaje hili wazo la masoud kipanya la kutengeneza gari linalotumia umeme ili kuendelea mbele zaidi na hiyo ndiyo kuonesha kuthamini kile ambacho mtu anachokibuni na kukithamini kwaajili ya tija, siyo ya kwake tu bali ya familia lakini pia na ya nchi kwasababu gari linapotoka limeandikwa ‘Made in Tanzania’ tunaitangaza nchi, tunatangaza ubunifu wa nchi lakini pia linatusaidia kuleta fedha ya kigeni nchini”alisema 

Aidha Chongolo alimuhakikishia   Kipanya kuwa atasimamia Mchakato mzima wa kufanikisha mchango kwa Taasisi mbalimbali kuwezesha ubunifu aliouanzisha ili kutoka katika hatua ya sasa na kwenda katika hatua nyingine mbele

“Ni lazima tuwe na mazingira ya kuchangiana kwenye masuala ya msingi, na mimi nitalisimamia suala hili la kukuchangia kiwango ambacho hakitopungua Milioni 100 , kwasababu tuna wadau na marafiki ambao watawezesha suala hilo, tutachanga hata kama fedha haitokwenda kutoa matokeo makubwa lakini kitendo Cha kwenda kutoa matokeo fulani kitaleta tija kubwa na hatua kubwa,”alisema 

Pia Chongolo alisema kuweka mazingira wezeshi katika kuheshimu na kuthamini mawazo ya ubunifu na ufundi itachochea na kukuza sekta mbalimbali nchini hasa sekta ya viwanda.

Kwa upande wake Mbunifu wa gari KP Motors , Kipanya alisema lengo la ubunifu huo ni kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazozalisha magari na kuuza nje ya nchi kwa kutumia malighafi zilizopo nchini.

Aidha Kipanya  alisema kupitia gari hilo tayari Kuna kundi kubwa la watanzania ambao wamehamasika kunyanyuka na kuendelea na vumbuzi na bunifu mbalimbali ambapo wamekuwa wakizifanya

Kipanya alisema Ujio wa viongozi mbalimbali  wa serikali na Chama katika kiwanda chao  unazidi kuonesha kwamba vitu vinavyofanywa na wabunifu vinaonekana.

Kwa upande wake Meneja shirika la viwanda vidogo SIDO Mkoa wa Dar es salaam ,Ridhiwani Matange alisema shirika hilo limekuwa likisaida wabunifu kukuza sekta ya viwanda na uzalishaji kwa kuthamini ubunifu na ufundi kwa maendeleo ya nchi ambapo kwa upande wa kiwanda Cha Masoud kipanya wamewapa eneo,  mawazo ya namna ya kuboresha ili kuendeleza ubunifu wake lakini pia kuendelea kumuunga mkono pale ambapo mazingira yanawezesha kwa ubunifu wake anaoufanya lengo aweze kuendelea mbele