April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ajira za Serikali zaidi ya 44,000 zamwagwa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI imetangaza ajira mpya 44,096 huku ikiwapandisha vyeo watumishi  92,619 pamoja na kubadilisha kada watumishi 6,026   kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Aidha ,utekelezaji wa Ajira hizo utaigharimu Serikali kiasi cha shilingi bilioni 26.297 kwa mwezi sawa na Shilingi bilioni 315.570 kwa mwaka.

Hayo yamesema jana jijini hapa na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Serikali  ya kuajiri watumishi wapya.

‘Kama mtakavyokumbuka katika mwaka wa fedha 2021/22 Serikali iliidhinishiwa nafasi 44,096  za ajira mpya, nafasi  92,619 za kupandisha vyeo watumishi  pamoja na kuwabadilishia kada/vyeo  watumishi 6,026 kwa kada mbalimbali.’alisema Mhagama na kuongeza kuwa

‘Kati ya nafasi 44,096  za Ajira mpya, Serikali kupitia Taasisi zinazotumia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara imeshaajiri watumishi  12,336  wakiwemo watumishi 11,492 wa ajira mpya na watumishi 844 wa ajira mbadala  hadi sasa na watumishi hawa wanaendelea kutekeleza majukumu yao katika taasisi mbalimbali za umma.’

Mhagama alisema,taarifa hiyo ni hatua ya kwanza ya mchakato wa kuhakikisha utekelezaji wa ajira hizo unakamilika kabla ya mwaka wa fedha 2021/22 haujaisha.

‘Kwa kutambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha Taifa linapata maendeleo ya haraka ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya ujenzi wa uchumi na inayotoa huduma iliyoasisiwa na Serikali zilizopita na ile iliyoanzishwa na inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Miradi ya UVIKO 19, Serikali imetoa kipaumbele katika Sekta za Elimu, Afya. ‘alisisitiza na kungeza kuwa
‘‘Pamoja na Sekta hizo, Serikali imezingatia mgawanyo wa ajira katika Sekta nyingine zikiwemo Kilimo, Maji, Mifugo, Uvuvi pamoja na maeneo mengine yenye uhitaji  wa watumishi ’’

Kuhusu watumishi wanaopandishwa vyeo Mhagama alisema, Serikali  pia itawapandisha vyeo/madaraja watumishi 92,619  ambapo  itatumia jumla ya Shilingi bilioni 23.078 kwa mwezi sawa na Shilingi bilioni 276.938 kwa mwaka na kuwabadilisha vyeo/kada (Recategorization) watumishi 6,026 waliotengewa Ikama na Bajeti ya Mishahara kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 kuanzia Mei Mosi mwaka huu  kwa gharama ya Shilingi milioni 824. 441 kwa mwezi sawa na Shilingi bilioni 9.893 kwa mwaka.

‘‘Kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan  jumla ya watumishi wa umma 282,400 watakuwa wamepandishwa vyeo katika kipindi hiki kifupi…., Aidha, jumla ya watumishi 25,412 watakuwa wamebadilishiwa kada katika kipindi tajwa.’’

Wa

Ameziagiza Mamlaka za Ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Afya pamoja na Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanaendesha michakato ya ajira hizo kwa uwazi, weledi, uadilifu pamoja na kutoa fursa sawa kwa waombaji wote kuweza kushiriki katika mchakato huo na hatimaye Serikali iweze kupata watumishi mahiri na wenye sifa stahiki.

Aidha amewataka waajiri kutotumia fursa hiyo kuajiri watumishi wazembe au wasiotekeleza majukumu yao kikamilifu kwa lengo la kujaza nafasi kwani jambo hili halikubaliki na halitavumiliwa kwa namna yeyote.

Alisema, Ofisi yake itafuatilia mchakato mzima wa ajira hizo hatua kwa hatua ili kuhakikisha Serikali inapata watumishji wenye sifa na ubora ambao wapo tayari kulitumika Taifa.