May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri Jiji la Mbeya yamkabidhi magari mawili Mkandarasi mshauri wa mradi

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Mbeya,DorMohamed Issa amekabidhi magari mawili aina ya Toyota Hillux Double Cabin kwa mhandisi mshauri wa mradi wa TACTIC kwa ajili ya usimamizi wa miradi .

Hatua ya kukabidhi magari hayo ni kutokana na ujenzi wa Barabara, mitaro ya maji ya mvua, ujenzi wa soko la sokomatola,ujenzi wa stendi kuu ya Mkoa ya mabasi, ujenzi wa jengo la maabara ambalo ndani yake kutakuwa na ofisi ya usimamizi wa mradi huo.

Akikabidhi magari hayo Mei 6,2024 Issa ametaja mkandarasi kusimamia vizuri vitendea kazi hivyo vilivyotolewa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Aidha Issa amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Dkt.Tulia Ackson kwa ufuatiliaji wake mzuri katika kuhakikisha kuwa analeta maendeleo kwa Wana Mbeya katika kutatua changamoto mbalimbali za miundombinu.

“Ndugu yangu Mhandisi kwa niaba ya Halmashauri nakukabidhi magari haya ambayo yatakuwa ni kitendea kazi kikubwa kwenye kazi yako tunaamini kabisa utakuwa karibu na mkandarasi katika usimamizi wa utengenezaji wa barabara zetu ili kuondoa changamoto ya miundombinu ya barabara kwenye maeneo ambayo barabara zitawekwa lami”amesema Mstahiki Meya.

Hata hivyo Issa amesema Magari hayo yamenunuliwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ambayo thamani yake ni shilingi milioni 231,885,835.18 na kusema yameletwa Jijini Mbeya kwa ajili ya usimamizi wa mradi wa TACTIC ili yaweze kurahisisha kazi ya utengenezaji wa miundombinu yote itakayotengenezwa kupitia mradi huo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa magari hayo ,Mhandisi Mshauri wa mradi wa TACTIC, Mhandisi wa mradi Geofrey Kanjanja ameishukuru Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa kuwakabidhi magari mawili na kuahidi kuyasimamia magari hayo.

Mradi wa TACTIC ni miongoni mwa miradi mikubwa nchini ya uboreshaji wa miundombinu unao tekelezwa katika Halmashauri 45 huku kwa awamu ya kwanza ukianza na Halmashauri 12 ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambayo itatengeneza barabara, mitaro ya maji ya mvua pamoja na maabara yenye ofisi za wahandisi wajenzi wa mradi.