April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya EQUITY yaja na KARIBU MEMBA

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Benki ya Equity kwa kushirikiana na Taasisi zinatoa ushirikiano kwenye kilimo ikiwemo YARA na AGRICOM imeendelea kutoa elimu ya fedha kwa mkulima ili kumsaidia mkulima kupata huduma zilizo nafuu.

Hayo ameyasema leo (Jun 1, 2022) Jijini Dar Es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji Benki ya Equity, Rojas Mdoe akimuwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Equity Benki, Isabel Maganga wakati wa uzinduzi wa kampeni ya KARIBU MEMBA ambayo ni kwaajili ya kuanza kusherehekea miaka kumi ya utoaji huduma kwa watanzania.

Mdoe amesema ndani ya miaka kumi Benki ya Equity imeweza kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya 430 na kubadilisha maisha ya watanzania zaidi ya 500,000 kiuchumi na kijamii;

“Tunahudumia watanzania zaidi ya laki tano mpaka sasa na tunategemea kuongeza zaidi lakini pia tumehudumia kuanzia ngazi ya chini kabisa kwa wafanyabiashara wadogowadogo wakiwemo wakulima, kutoa huduma mbalimbali za kifedha ikiwa ni pamoja na utunzaji wa fedha, akaunti za watoto, vikundi, mikopo mbalimbali kama ya wakulima, wastaafu, wafanyabiashara kubwa na ndogondogo, waajiriwa n.k”

Mbali na hayo, Mdoe amesema katika kuunga mkono serikali kuhakikisha wanaipa nguvu sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi wa nchi, hivi karibuni waliweza kuzindua mradi na taasisi mbalimbali kwaajili ya mikopo ya wakulima

Aidha Mkuu huyo wa kitengo wa Benki ya Equity alisema mikopo yao ina riba nafuu ambayo inatolewa katika ngazi zote za kilimo, kwa mkulima anaelima mwenyewe, kwa yule anaesambaza pembejeo, anaeingiza pembejeo na anaenunua mazao;

“Mikopo yetu ya kilimo riba yake ipo kuanzia 8% mpaka 15% kulingana na ngazi katika mnyororo wa thamani lakini pia uwezo wa yule anaekopeshwa na uwezo wake wa kifedha wa kuweza kuhudumia lakini pia uzalishwaji wake kwasababu riba ni sehemu ya mchango katika uzalishaji wa mkopeshwaji”

Mkuu huyo wa kitengo amesema, Miongoni mwa changamoto zilizopo katika sekta ya kilimo ni umilikaji wa mali na utambulisho hivyo amewashauri watengeneze vikundi ili kuwa rahisi kwa Benki kuwatambua.

Mdoe amesema Benki hiyo imejikita katika kutatua changamoto za wananchi na itaendelea kutoa elimu na fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki kwa Memba wa Tanzania na Dunia kwa ujumla