April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Askari Polisi watunukiwa vyeti,wasisitizwa kufanya kazi kwa weledi

Na. Mwandishi wetu,Arusha

JESHI la Polisi Wilaya ya Kipolisi Murieti Jijini Arusha limetunuku vyeti vya sifa na pongezi kwa askari wake waliofanya vizuri zaidi kwa mwaka 2023 huku wakisisitizwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi katika kuwahudumia wananchi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Polisi Wilayani humo Mrakibu wa Polisi SP Pius Msaki Machi 02, 2024 wakati wa usiku wa sherehe iliyoandaliwa kwa ajili ya kutoa vyeti vya sifa na zawadi kwa askari waliofanya vizuri zaidi kwa mwaka 2023.

SP Msaki pamoja na kuwashukuru Askari kwa kumkaribisha mara baada ya kuhamia katika wilaya hiyo lakini pia kuwapongeza Askari waliofanya vizuri, amesema ni wajibu wa kila Askari Polisi kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaimarika wakati wote hasa kwa kuzingatia Mkoa huo ni Kitovu cha Utalii hapa Nchini.

Naye Mdau wa Masuala ya Usalama Bwana Innocent Moshi ambaye alikua mgeni Maalum katika hafla hiyo amelipongeza Jeshi la Polisi Wilayani humo kwa namna ambavyo wamekua wakiimarisha usalama wa Raia na Mali zao huku akiahidi kuwa ataendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo pindi utakapohitajika.

Mkuu wa Kituo cha Polisi Murieti Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Tausi Mbalamwezi amebainisha kuwa Jeshi hilo lina utaratibu wa kuwatambua na kuwapongeza Askari wanaofanya vizuri zaidi kila mwaka ambapo katika hafla hiyo jumla ya Askari watano walipokea vyeti vya pongezi kwa kufanya vizuri zaidi mwaka 2023 Wilayani humo.

Naye Sajenti Wito Ntope kwa niaba ya Askari waliofanya vizuri zaidi pamoja na kushukuru Jeshi hilo kutambua na kuthamini utendaji wao, alisema vyeti na zawadi walizopewa zitaongeza chachu na morali katika utendaji wao wa kazi huku akiwataka Askari wengine kufanya kazi kwa uadilifu na kutenda haki kwa wananchi wanaowahudumia.