April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea urais upande Tanzania Bara,Queen Sendiga akikabidhiwa ilani ya chama hicho.

ADC kuongeza ajira milioni 10 kwa kipindi cha miaka mitano

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Pemba

CHAMA cha Allance for Democratic Change (ADC),kimesema endapo Watanzania watakipa ridhaa ya kuongoza kitahakikisha kuwa kinaongeza ajira zaidi ya milioni kumi katika kipindi cha miaka mitano.

Hayo yalibainishwa kwenye ufunguzi wa kampeni zake pamoja na ilani uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja Zanzibar na kuhudhuriwa na wagombea urais upande Tanzania Bara,Queen Sendiga na mgombea urais Zanzibar Hamad Rashidi Mohamed ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha ADC Taifa.

Mgombea urais upande Tanzania Bara,Queen Sendiga akikabidhiwa kipeperushi cha sera na ilani ya chama hicho.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Queen amesema kuwa ADC imejiwekea malengo mbalimbali endapo wananchi watakipa ridhaa ya kuongoza nchi.

“Tumejiwekea mipango madhubuti ambayo kama wananchi wataupa ridhaa ya kuongoza basi manufaa makubwa watayapa ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira,” amesema.

Amesema kuwa ADC ina vipaumbele vyake vya kuhakikisha kuwa inasimamia ipasavyo ili wananchi wananufaika kupitia elimu ,kilimo kwani watapa ajira kutokana na sekta hizo.

Amesema kuwa ajira hizo zinatokana na kilimo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wananchi kupata mikopo yenye riba nafuu katika taasisi za fedha ili wawe na kilimo chenye tija.

“Kwenye kilimo kuna matawi mengi kama ufugaji, uvuvi ambapo katika sekta ya ufugaji itaboreshwa kitaalam ili ufugaji uwe na tija,” amesema.

Queen amesema kuwa ADC itaondoa kabisa tatizo la ajira kwa wanafunzi wanaomaliza vyooni kwani watakwenda kwenye sekta ya kilimo ambayo itaboreshwa na kuwa kimbilio la wengi.

Mgombea urais huyo amesema kuwa endapo ADC itaingia madarakani Serikali itaweka Mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwepo na viwanda vinavyopandisha thaman mazao ya mifugo, kwa kufanya hivyo mifugo itakuwa na thamani kubwa.

“Tunaamini kuwa kwa kuboresha hayo tutakwenda kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kuongeza ajira kupitia sekta ya mifugo.

“Serikali ya ADC inakwenda kuwahimiza wanachi wanaoishi katika maeneo yenye uvuvi kuwa katika vikundi ili kukopeshwa vitendea Kazi ili waweze kuwa na uvuvi wenye tija,” amesema.

Mgombea urais Tanzania Bara Queen Sendiga akizungumza kwenye mkutano wa kampeni.

Naye mgombea urais Zanzibar Hamad Rashidi Mohamed amesema kuwa kuhusu uvuvi wa bahari kuu Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itanunua meli kubwa ya uvuvi ili kuwepo na uvuvi mkubwa katika bahari kuu hivyo kwa kufanya hivyo kutainua uchumi na kuanzisha ajira mpya

Naye meneja kampeni wa ADC Devilsi Method amesema kuwa Septemba kesho chama hicho kinatarajia kuzindua kampeni zake
Mjini Pemba – Zanzibar,viwanja vya Shame Mmata, Soko la mjini micheweni.

“Tunawaomba wananchi watupe ridhaa ya kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka mitano wataona manufa amakubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kubwa,” amesema.

Amesema kuwa mara baada ya hapo kitaendelea kuzunguka katika maeneo mbalimbali nchini.