March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lissu ashindwa kufika mahakamani, kisa kampeni

Na Esther Clavery -Tudarco

KESI ya uchochezi, inayowakabili mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kuendelea na usikilizwaji kwa sababu ya kampeni za uchaguzi Mkuu unaoendelea hapa nchini.

Lissu anadaiwa kuwa kwenye kampeni, ambapo wadhamini wake walishindwa kumpata ili kumleta mahakamani kama sheria inavyoelekeza.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa na kwamba washtakiwa wawili ambao ni Lissu na Jabir Idrisa hawapo mahakamani.

Baada ya kueleza hayo, Mdhamini wa Lissu, Robert Katula alidai kuwa amewasiliana na watu wa karibu wa mshtakiwa huyo (Lissu) na kumueleza kuwa yupo kwenye kampeni kuelekea uchaguzi Mkuu.

“Ulisema leo (jana) tuje naye, nimejaribu kuwasiliana naye sijampata hadi sasa hivi, amebanwa na ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hivyo tunaomba Mahakama ipange tarehe nyingine,” alidai Katula

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi kesho 15, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa. Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Wahariri wa gazeti la Mawio,Simon Mkina na Jabir Idrisa pamoja na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu na wenzake wanakabiliwa na mashitaka matano ikiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.