October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa Taifa CHADEMA, Freeman Mbowe

Vikao vya kumpata mgombea Urais CHADEMA kuanza kesho

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)imetoa ratiba ya vikao vya ndani vya Chama hicho ambavyo vitahitimishwa kwa kufanya uteuzi wa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgombea mwenza na mgombea wa urais wa Zanzibar.

Vikao hivyo vinavyotarajia kuanzia kesho Agosti 2 hadi 4, 2020, katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es salaam.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa CHADEMA, Tumaini Makene imesema vikao hivyo vya kitaifa ambavyo ni Kamati Kuu ya Chama, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu, vitaketi kwa siku tatu mfululizo na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Chama ya Mwaka 2006, Toleo la Mwaka 2019.

“Kikao cha kwanza kitakuwa ni Kamati Kuu ya Chama itakayokutana Jumapili, Agosti 2, mwaka huu, itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba unaoelekezwa kwenye ibara ya 7.7.16(a) “Kufanya utafiti wa wagombea wa urais na mgombea mwenza na kuwasilisha ripoti zake kwa Baraza Kuu,”imesema taarifa hiyo,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Agosti 3, 2020, Baraza Kuu la Chama litakutana katika kikao chake, ambapo litajadili masuala mbalimbali ikiwemo “kufanya mapendekezo ya wagombea wa Urais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na kuyawasilisha katika Mkutano Mkuu kwa uamuzi.

Kwa mujibu wa ibara ya 7.7.12 (n) Baraza Kuu litajadili rasimu ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu na kuwasilisha mapendekezo yake kwa Mkutano Mkuu kwa maamuzi,”imesema

Aidha taarifa hiyo imesema Agosti 4,2020, Mkutano Mkuu wa Chama utaketi na kutekeleza kazi zake, ikiwemo “kuteua mgombea wa Urais na mgombea mwenza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais wa Zanzibar kama inavyoelekezwa kwenye ibara ya 7.7.10 (c).

Halikadhalika, Mkutano Mkuu wa Chama utainidhinisha Ilani (manifesto) ya Chama kwa Uchaguzi Mkuu, kwa mujibu wa ibara ya 7.7.10 (h).