August 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima Mbarali watakiwa kutanua Kilimo cha Korosho

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya

MBUNGE wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya, Bahati Ndingo, amewataka wakulima wilayani humo kutanua wigo wa mazao wanayolima kwa kuingia katika kilimo cha korosho, badala ya kutegemea zao la mpunga pekee.

Ndingo amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza vyanzo vya mapato kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kaya na wilaya kwa ujumla.

Mbunge huyo ametoa kauli hiyo Agosti 8, 2026, wakati alipotembelea mabanda ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali katika maadhimisho ya kilele cha sherehe za Nane Nane za Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, zilizofanyika jijini Mbeya.

Amesema licha ya mpunga kuwa zao kuu la chakula na biashara kwa wakazi wengi wa Mbarali, kuna fursa nyingine za kilimo ambazo wakulima wanapaswa kuzitumia kuongeza kipato.

“Leo nimepita kutembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali. Kitu kilichonivutia ni kuona wana Mbarali wamezoea kulima mpunga, ambao ni zao la biashara na chakula, lakini pia sasa tuna mazao mengine yanayokwenda kuongeza tija katika Halmashauri yetu na kwa jamii nzima ya wana Mbarali,” amesema.

Ndingo amesema wakulima wanapaswa kutumia fursa zilizopo katika kilimo cha mazao mbalimbali ya biashara, ikiwamo korosho, ili kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Amewataka pia wananchi kutumia maeneo madogo waliyonayo kuzalisha mazao ya bustani kwa ajili ya chakula na biashara.

“Ndugu zangu wananchi wa Mbarali, pia limeni kilimo cha mbogamboga kwa kutumia eneo dogo. Kwa kufanya hivyo, mtaweza kupata mazao yenye tija ambayo yataweza kusaidia mahitaji ya nyumbani na pia kuongeza kipato,” amesema.

Amesema tayari kata 12 katika Wilaya ya Mbarali zimeanza kulima korosho, akieleza kuwa mwitikio wa wakulima ni mkubwa na Serikali inaendelea kutoa elimu kuhusu zao hilo.

Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbarali, Sadock Mpangile, amesema kilimo cha korosho kinaendelea kupewa msukumo kutokana na fursa kubwa ya kiuchumi inayoweza kupatikana kwa wakulima watakaokifanya kwa tija.

Mpangile amesema wilaya hiyo ina maeneo yanayofaa kwa kilimo cha korosho na kwamba Serikali imekuwa ikitoa miche kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

“Kwa Wilaya ya Mbarali karibu maeneo yote yanafanya vizuri. Karibu kila mwaka Serikali inatoa miche 60,000 kwa ajili ya wakulima,” amesema.

Amesema ongezeko la wakulima wanaojihusisha na kilimo cha korosho linaonesha kuwa zao hilo linaendelea kupata umaarufu katika wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbarali, Mary Mbwilo, amewataka maafisa kilimo kuongeza elimu kwa wakulima kuhusu kilimo cha korosho na mazao mengine ya biashara.

Mbwilo amesema elimu hiyo itawasaidia wakulima kutambua fursa zilizopo katika mazao mbalimbali na kuondokana na utegemezi wa zao moja pekee.

Amesema wakulima wanapaswa kutumia fursa za kilimo cha mazao yenye thamani kiuchumi ili kuongeza kipato cha familia na kuchangia maendeleo ya wilaya.