June 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampeni ‘Kila muamala bao laushindi’ yazinduliwa Zanzibar

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online

KAMPUNI ya Mixx kwa kushirikiana na Hisense imeendelea na uzinduzi wa kampeni yake ya ‘Kila Muamala ni Bao la Ushindi’ visiwani Zanzibar, baada ya uzinduzi rasmi uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha, amesema kampeni hiyo imezinduliwa wakati ambao hamasa ya Kombe la Dunia inaendelea kuongezeka miongoni mwa Watanzania, ambao wengi wana mapenzi makubwa na mchezo wa mpira wa miguu.

“Mpira wa miguu una uwezo wa kuunganisha watu kwa namna ya kipekee. Kuelekea Kombe la Dunia, tumeona ni wakati sahihi wa kusherehekea pamoja na wateja wetu kwa kuwapa fursa ya kushinda zawadi zinazoweza kubadili maisha,” amesema Pesha.

Ameongeza kuwa, kampeni hiyo pia inalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za fedha kidijitali huku ikitoa motisha kwa wateja kupitia zawadi mbalimbali zitakazotolewa katika kipindi chote cha kampeni.

“Kila muamala unaofanyika unaweza kuwa mwanzo wa ushindi mkubwa kwa wateja wetu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” amesema.

Kupitia kampeni hiyo, Mixx inatoa zawadi za shilingi milioni moja kila siku, Zawadi za vifaa vya kielektroniki kutoka Hisense ikiwemo Televisheni ya inchi 55, spika za muziki pamoja na majokofu ya milango miwili.

Katika zawadi kubwa zaidi za kampeni hiyo, washindi watano watasafirishwa kwenda Mexico kushuhudia mechi za Kombe la Dunia mubashara huku gharama zote zikigharamikiwa kikamilifu.

Aidha, mshindi mmoja wa droo ya mwisho wa kampeni ataibuka na kitita cha shilingi milioni 50.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Mars Communications Ltd, wasambazaji wa vifaa vya Hisense nchini, Tahera Karim amesema ushirikiano kati ya Hisense na Mixx unalenga kuwapa Watanzania thamani zaidi kupitia zawadi za teknolojia ya kisasa.

“Tunafurahi kushirikiana na Mixx katika kampeni hii inayowawezesha Watanzania kushinda zawadi zenye thamani kubwa huku wakitumia huduma wanazozihitaji kila siku.

“Kupitia Hisense, tunatoa bidhaa za teknolojia ya kisasa zinazoboresha maisha ya watumiaji, na tunaamini kampeni hii itawagusa watu wengi zaidi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” amesema.

Kwa mujibu wa Mixx, kampeni hiyo itakayodumu kwa muda wa miezi miwili inawahusisha watanzania wote watakaotumia huduma mbalimbali za Mixx ikiwemo kutuma fedha kutoka Mixx kwenda Mixx.

Lakini pia, kufanya malipo kupitia Lipa kwa Simu, kulipa bili, kufanya miamala ya michezo ya kubashiri, kuwekeza katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) pamoja na kutumia huduma za Mixx Super App.

Wadau wa sekta ya fedha wameeleza kuwa kampeni za aina hiyo zina mchango katika kuchochea matumizi ya huduma za fedha kidijitali, hususan kwa wafanyabiashara wadogo na wananchi wanaotegemea huduma za simu katika shughuli zao za kila siku.

Mixx imesema, itaendelea kuwekeza katika huduma za kidijitali zinazowarahisishia Watanzania kufanya miamala kwa usalama, urahisi na kwa gharama nafuu, huku kampeni hiyo ikitoa motisha ya ziada kwa watumiaji wake.

Kwa wakazi wa Zanzibar, kampeni hiyo inafungua fursa mpya za ushindi kupitia miamala ya kawaida ya kila siku, huku ikiongeza hamasa ya Kombe la Dunia kwa maelfu ya watumiaji wa huduma za Mixx visiwani humo.