August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahamasishwa kutumia mbegu bora za mifugo kuongeza tija

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Arusha

WAFUGAJI nchini wamehimizwa kuwekeza katika matumizi ya mbegu bora za mifugo ili kuongeza uzalishaji wa nyama, kuboresha ubora wa mifugo na kuongeza kipato, badala ya kuendelea kufuga mifugo yenye vinasaba duni ambayo imekuwa ikichangia uzalishaji mdogo.

Rai hiyo ilitolewa Agosti 5,2026 na Meneja wa Shamba la West Kilimanjaro Ranch,Adil Butt wakati wa Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Njiro, mkoani Arusha, ambapo kampuni hiyo inashiriki kuonesha mifugo ya kisasa na teknolojia za ufugaji.

Butt amesema ushiriki wa kampuni hiyo unalenga kuwahamasisha wafugaji kufuga mifugo yenye tija kwa kutumia mbegu bora zinazoweza kuongeza uzalishaji wa nyama na kuinua kipato cha wafugaji.

 Amesema wameleta aina mbalimbali za mifugo ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo ili wananchi wajifunze kuhusu mifugo inayofaa kwa mazingira ya Tanzania.

Ameeleza kuwa upande wa ng’ombe wamewasilisha aina ya Boran, yenye asili ya Kenya, ambayo inaweza kufikia uzito wa zaidi ya kilo 800, pamoja na aina nyingine zikiwemo Simmental na Tuli zinazofugwa katika shamba lao.

Kwa upande wa kondoo,amesema wameleta aina za Meatmaster, Dorper, Red Maasai na Persian Blackhead kutoka Namibia kwa lengo la kuongeza vinasaba bora nchini na kupunguza changamoto ya kuzaliana kwa ukoo mmoja (inbreeding).

Aidha,amesema baadhi ya mifugo hiyo imetoka Namibia na Afrika Kusini na imechaguliwa kutokana na uwezo wake wa kustahimili mazingira ya Tanzania, hususan maeneo yenye ukame.

Butt amesema katika kipindi cha miezi sita tangu waanze shughuli zao wamepokea mwitikio mkubwa kutoka kwa wafugaji wanaotembelea shamba lao, huku changamoto kubwa iliyobainika ikiwa ni upatikanaji wa malisho bora.

Amefafanua kuwa West Kilimanjaro Ranch ipo eneo la Sanya na ilianza shughuli zake rasmi mwaka 2024 ikiwa na dhamira ya kusambaza mbegu bora za mifugo kwa wafugaji nchini.

Amebainisha kuwa kampuni hiyo inatekeleza programu maalumu ya kuboresha vinasaba vya mifugo kwa kushirikiana na jamii, ambapo vikundi vya wafugaji vitasajiliwa na kupewa huduma za madume bora ili kuboresha mifugo yao.

Pia amesema kampuni inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Uzalishaji wa Mbegu na Viinitete (Embryo and Semen Center), ambacho kitarahisisha upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora za mifugo kupitia wataalamu wa mifugo.

Kwa mujibu wa Butt, kampuni hiyo inatumia zaidi ya hekta 2,500 za ardhi zilizotolewa kupitia NARCO kwa ajili ya kuendeleza ufugaji wa kisasa na kuzalisha mifugo bora.

Ameongeza kuwa hadi sasa kampuni imeajiri zaidi ya wafanyakazi 210 kutoka katika jamii zinazozunguka eneo hilo, wakiwemo wanawake zaidi ya 50, hatua ambayo alisema  imechangia kuongeza ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi katika maeneo husika.